Majaliwa akataa gharama ujenzi nyumba za walimu

IRINGA; Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezuia mpango wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi katika shule ya Sekondari Ilamba kutumia makadirio ya Sh Milioni 100 kujenga nyumba mbili katika moja ya walimu, akisema gharama hiyo imekuzwa.

Pamoja na agizo hilo alilolielekeza kwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo na madiwani wenzake, Waziri Mkuu amekagua na kuyakataa madawati yote ya shule hiyo mpya ya wasichana, ambayo hayana droo za kuwekea daftari na vitabu vya wanafunzi.

Advertisement

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ilamba baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule hiyo inayoendelea kujengwa, Majaliwa alisema yupo katika ziara ya siku tatu mkoani Iringa kukagua utekelezaji wa Ilani na miradi mbalimbali iliyoahidiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Ninapoondoka hapa, nataka madawati yote yasio na droo hizo yaondolewe na kurudishwa kwa fundi,” alisema.

Akizungumzia gharama za ujenzi wa nyumba za walimu alisema makadirio ya serikali yanataka nyumba moja ya mwalimu yenye vyumba vitatu vya kulala ijengwe kwa kati ya Sh Mioni 25 na Sh Milioni 30.

“Sasa ninyi mnataka kutumia Sh Milioni 100 ambayo kwa ramani ya serikali inatoa nyumba tatu kujenga nyumba mbili tena katika moja ambayo gharama yake inaweza kupungua,” alisema.

Aliiagiza halmashauri hiyo kupitia upya gharama za ujenzi wa nyumba hizo, ili ziendane na gharama halisi inayotakiwa kutumiwa.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa shule hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa alisema hadi kukamilika kwake shule hiyo iliyoanza kujengwa April, 2023 itagharimu zaidi ya Sh Bilioni 1.7.

Taarifa ya halmashauri hiyo inaonesha shule hiyo hiyo itakuwa na vyumba 21 vya madarasa (nane vimekamilika) kikiwemo chumba cha kompyuta, jengo la utawala, maabara tatu na mabweni manne.

Majengo mengine ni bwalo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400, matundu ya vyoo na nyumba tano za walimu ambazo Waziri Mkuu ametilia shaka ujenzi wake.