640 wapata ufadhili wa masomo wa Samia

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kesho inatarajia kutangaza majina ya wanafunzi 640 wanaostahili kupata ufadhili wa masomo kupitia Samia Scholarship baada ya kufanya vizuri masomo ya sayansi.
Waziri wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda alisema Jumapili jijini Dodoma kuwa katika kupata ufadhili huo hakutakuwa na upendeleo au ushawishi.
“Septemba 27, 2022 (kesho) tunafungua rasmi tangazo la wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kufanya mitihani kupitia Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) na kufaulu vizuri kwenye masomo ya sayansi ambao wanastahili kupewa Samia Scholarship, baada ya hapo majina yao yatatangazwa.” alisema Profesa Mkenda wakati wa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu kufungua tangazo la Samia Scholarship.
Aliongeza “Kwa wanafunzi ambao wamefanya vizuri sana katika masomo ya sayansi ambao wanastahili kupewa Samia Scholarship tunayo majina 640, tutangaza.”
Profesa Mkenda alisema moja ya kigezo cha kupata ufadhili ni mwanafunzi kudahiliwa kwenye vyuo vikuu vya ndani ya nchi kusoma masomo ya sayansi, uhandisi na elimu tiba.
Alisema kwa mwanafunzi ambaye atadahiliwa kwenye masomo ambayo si ya sayansi hawatanufaika na ufadhili huo hata kama jina lipo kwenye orodha ya walio na sifa ya kupata.
“Unaweza ukawa umefaulu masomo ya sayansi na ukawemo kwenye orodha tutakayoitangaza lakini umeenda kwenda kusoma nje ya nchi kwa mtu anakusomesha basi utakosa fursa hii”alisema profesa Mkenda na kuongeza;
“Pia unaweza jina lako likawepo na umedahiliwa katika chuo kikuu hapa Tanzania nje ya masomo ya sayansi, uhandisi na elimu tiba utakosa fursa hiyo”
Aliongeza “Kikubwa mwanafunzi awe umefaulu masomo ya sayansi, hakuna lobbying matokeo ya nani kafauli vizuri yako wazi na kila mtu anaweza kuona, kwa hiyo hakuna cha kusema mtoto wa Mkenda au Silvia, hapana ulichofaulu ndio kitakufanya uchaguliwe.”
Profesa Mkenda alisema Wizara imetanga Sh bilioni tatu ambazo zinaweza kuwatosha wanafuzi 640 kwa mwaka wa kwanza.
“Tutakapoingia mwaka wa pili inaweza kuwa shilingi bilioni sita na zitaendelea kuongezeka kulingana na uhitaji, hapa tutazindua tangazo lakini uzinduzi wa hii scholarship yenyewe tumemuomba Rais akutane na hao watakaokuwa wamekamilisha vigezo vyote.”alisema.
Mbona siyaoni majina ya hao wanafunzi waliofadhiliwa