78 wafa wakisubiri msaada wa Ramadhani

WATU 78 wamekufa na wengine 13 wamejeruhiwa baada ya kutokea vurugu kwenye shule moja katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa wakati walipokuwa wakisubiri kupokea msaada wa mwezi wa Ramadhani.

Inaelezwa kuwa maelfu ya watu walikusanyika katika shule ya Maeen jijini humo wakisubiri kupatiwa msaada wa dola tisa za Marekani kwa kila mmoja kabla ya kukutwa na kadhia hiyo iliyotokana na mkanyagano.

Tukio hilo linahusishwa na kundi la wanaharakati waasi wa Houthi ambalo limekuwa likiushikilia mji wa Sanaa tangu mwaka 2015.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo, wafanyabiashara wakubwa wawili mjini humo  wanashikiliwa na mamlaka za usalama na uchunguzi bado unaendelea.

Msemaji wa Wizara hiyo alilaumu vitendo vya kugawa misaada kwa watu wengi bila kushirikisha mamlaka za kiserikali.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa wapiganaji wa Houthi walifyatua risasi hewani wakijaribu kutawanya kusanyiko hilo na kusababisha mlipuko baada ya kupiga waya za umeme hali iliyosababisha taharuki na kuzua hamaniko hilo.

Inasemekana waasi hao waliifunga shule hiyo na kuzuia watu wote ikiwemo waandishi wa habari kutokaribia eneo hilo na waliripotiwa kukubali kulipa kiasi cha dola za Marekani 2,000 kwa kila raia aliyepoteza ndugu katika vurugu hizo na dola 400 kwa majeruhi.

Wakati huo huo mamlaka nchini Yemen ziko katika juhudi za kumaliza mzozo nchini humo ambapo wiki iliyopita kulifanyika mabadilishano ya wafungwa kwa pande mbili zinazopingana ikiwa ni moja ya hatua muhimu za mpango wa kumaliza mgogoro uliodumu kwa takribani miaka minane.

Habari Zifananazo

Back to top button