WMA Misugusuru yawa ya mfano kwa Afrika Mashariki
KITUO cha Wakala wa Vipimo (WMA) Misugusuru Mkoa wa Pwani kimekuwa cha mfano na nchi za Afrika Mashariki zimekuwa zikija kujifunza ubora wa kazi zinazofanywa kwenye kituo hicho.
Kituo hicho kimekuwa kikitumika kuhakiki ujazo wa mafuta kwenye malori, mita za maji na umeme na kilijengwa kwa gharama ya Sh bilioni saba.
Hayo yalisemwa jana na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, iliyotembelea kituo hicho.
Alisema kituo hicho ni kipya na kimekuwa mfano bora kutokana na kazi zinazofanywa kiasi cha kuvutia watu wa nchi jirani kuja mara kwa mara kujifunza kuhusu vipimo.
“Kituo hiki kinafanya kazi nzuri na kitaendelea kuwa mfano hivyo tunaamini Rais (Samia Suluhu Hassan)Ha ataendelea kutupa fedha tujenge vituo kama hivi kwa kanda kama ambavyo kamati ya bunge imeshauri,” alisema.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Stela Kahwa, alisema wabunge wameona hatua kubwa iliyofikiwa lakini wameshauri kuwe na maabara inayotembea ili kwenda kukagua mita za maji na umeme kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, David Kihenzile alisema wameona namna mita za maji zinavyohakikiwa na zile za umeme kuhakikisha mwananchi anapewa mita ya maji au umeme yenye ubora ili alipe kile tu anachotumia.
“Changamoto ambayo tumeiona ni kwamba hivi mtu anayetengeneza mita za maji Katavi au Shinyanga atazisomba zote aje zipimwe hapa Kibaha. Kwa hiyo tumewashauri wakala watazame haya mbeleni ikiwezekana vituo kama hivi vijengwe kwenye kanda lakini kwa kweli wanafanyakazi nzuri sana,” alisema.