WANAFUNZI 951 wa kidato cha nne katika Mkoa wa Mbeya, hawakufanya Mtihani wa kujipia (Mock) uliofanyika Julai Mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro, mimba na vifo.
Mtihani huo ulishirikisha mikoa yote ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambapo sababu zingine zilizowafanya wanafunzi hao kutofanya mtihani ni kuugua na sababu zingine.
Ofisa Taaluma wa Mkoa wa Mbeya, Ally Masoud alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa kikao cha wadau wa elimu kilichokuwa na lengo la kufanya tathimini ya elimu katika mkoa huo na kutangaza matokeo ya mtihani wa utimilifu.
Kikao hicho kiliwashirikisha wakuu wa shule, waratibu elimu kata, maofisa elimu wa halmashauri, wakurugenzi wa halmashauri, maofisa kutoka Chama cha Walimu nchini (CWT) na maofisa kutoka Ofisi ya Mdhibiti Ubora wa shule Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Masoud alisema kati ya wanafunzi hao ambao hawakufanya mtihani huo wavulana walikuwa 504 na wasichana 447 na wengi wao hawakufanya mtihani kwa sababu ya utoro.
Alisema wanafunzi 864 hawakufanya mtihani huo kwa sababu ya utoro, ugonjwa wanafunzi 50, vifo wanafunzi wawili sababu nyingine wanafunzi 12 na wasichana 23 hawakufanya mtihani kwa sababu ya kupata mimba.
Masoud alisema wanafunzi waliokuwa wamesajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa 26,726 lakini waliofanya walikuwa 25,775 ambao ni sawa na asilimia 96.44.
“Lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaokuwa wamesajiliwa kufanya mtihani wanafanya mtihani na wanafaulu vizuri, hawa wanafunzi ambao hawakufanya mtihani wana sababu mbalimbali na idadi inatofautiana kulingana na halmashauri,” alisema Masoud.
Alisema lengo la mkoa huo ni kufikia ufaulu wa asilimia 100 kutoka asilimia 89 ya mwaka jana na kupandisha ufaulu kufikia wa GPA ya 3.4 kutoka GPA ya 3.6 ya mwaka uliopita.
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya, Mwalimu Ernest Hinju aliagiza wakuu wa shule kwa kushirikiana na wadau wengine zikiwemo bodi za shule kuhakikisha wanafunzi wote ambao hawakufanya mtihani kwa sababu ya utoro wanafuatiliwa ili warejee shuleni.
Aliwataka kuhakikisha wanafunzi hao wanahudhuria shuleni siku zote zilizobaki kabla ya kufanya mtihani wa taifa ili kuepuka kuwa miongoni mwa watakaosababisha ufaulu kuwa chini ikilinganishwa na malengo ya Mkoa.
Alisema kwa sasa zimebaki siku zaidi ya 80 ambazo wanafunzi hao watatakiwa kukaa darasani na kusoma na wenzao ili kuepuka kushindwa tena kufanya mtihani wa mwisho.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera aliwataka walimu kufundisha kwa kuzingatia miongozo na mitaala ili kuhakikisha lengo la Serikali la kuzalisha wataalamu linafikiwa.
Homera aliwataka walimu kubadili mfumo wa adhabu kwa wanafunzi wanaofanya kazi kwa kuwapatia mitihani maalumu badala ya kuwapa adhabu ya viboko.