SERIKALI imewaagiza wawezeshaji wa kitaifa wanaoshiriki mafunzo ya kujenga ujuzi wa kuibua hadithi za mafanikio za kujifunza za mfano katika kuboresha ujifunzaji na ufundishaji, kuzingatia mafunzo hayo vyema na kuhakikisha yanaleta tija katika maeneo mengi nchini.
Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia , Dkt. Francis Michael leo tarehe 24/11/2022 mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya wawezeshaji wa kitaifa.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kupitia programu ya Shule Bora inayofadhiliwa na shirika la UKaid.
Dkt. Michael amesema, serikali imewekeza katika mafunzo ya walimu kazini, hivyo wanapaswa kuzingatia na kupeleka ujuzi waliopata kwa washiriki waliokusudiwa katika ngazi ya mkoa na halmashauri.
“Hakikisheni mnazingatia mafunzo haya na kushiriki kikamilifu ili kuendelea kushirikishana namna hadithi za mafanikio za kujifunza za mfano zinavyoweza kuboresha ujifunzaji na ufundishaji shuleni” amesema Dkt. Michael.
Pia amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujenga uhusiano mzuri na wadau wa maendeleo ya elimu nchini ambao wanaendelea kuwezesha kuwepo kwa miradi mingi ya elimu nchini.
Kwa upande wake Mshauri Mkuu kiongozi wa programu ya Shule Bora Vincent Katabalo amesema kuwa wataendelea kutekeleza mradi wenye lengo la kuongeza ubora wa elimu nchini.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amesema kuwa mafunzo hayo ni nyenzo muhimu kuleta ufanisi katika kutekeleza mitaala ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji darasani.