Aagiza miradi ya maendeleo Kondoa isimamiwe, ikamilike

KATIBU Tawala Mkoa wa Dodoma, Ally Gugu

KATIBU Tawala Mkoa wa Dodoma, Ally Gugu amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Mustapha Yussuf kuhakikisha miradi yote inayoendelea kutekelezwa katika hatua mbalimbali ikamilike ifikapo Mei 31, mwaka huu.

Gugu alitoa kauli hiyo wakati alipotembelea Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya sekta ya afya, elimu na utawala.

“Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Mustapha Yussuf hakikisha miradi yote inayoendelea kutekelezwa katika hatua mbalimbali ikamilike ifikapo 31, Mei mwaka huu,” alisema.

Advertisement

Miradi saba aliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa jengo la halmashauri, nyumba ya mkurugenzi na ujenzi wa nyumba tatu za watumishi.

Katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa, serikali imetoa Sh bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na makao makuu ya halmashauri katika eneo la Bukulu pamoja na ujenzi wa nyumba tatu za wakuu wa idara.

Gugu alitoa maelekezo kwamba mkurugenzi wa halmashauri hiyo ahakikishe miradi hiyo inakamilika kwa wakati kwa mujibu wa mkataba.

Aidha kuhusu sekta ya afya ambapo serikali kuu ilitoa Sh milioni 75 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya afya, Gugu alipongeza hatua nzuri ya maendeleo ya ujenzi wa majengo manne katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa likiwemo wodi la wanawake, wanaume, watoto na jengo la kuhifadhia maiti.

Gugu pia alitembelea mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kompyuta na ujenzi wa madarasa matatu katika Shule ya Msingi Isabe ambavyo gharama yake ni Sh milioni 80.

Akitoa maelekezo ya jumla baada ya kutembelea miradi ya sekta ya elimu na afya, Gugu alisema uongozi wa halmahauri unatakiwa kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika kwa muda uliopangwa na kwa ubora wa hali ya juu.

“Niwahikikishieni kuwa tutarudi tena, haya maelekezo tuliyowapa yazingatieni na tutakaporejea tupate taarifa ya utekelezaji wake kwa vitendo,” alisema.

Akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo, Gugu aliwataka kufuata misingi na taratibu za utumishi wa umma na kusisitiza kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *