Aapa kuwaweka pabaya wanaowapa mimba wanafunzi

MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Queen Sendiga ameapa kuwa walimu ‘wakware’ na wote wanaodaiwa kumaliza nje ya mahakamani mashauri ya mimba za wanafunzi siku zao zinahesabika, akionya kwamba hakuna atakayebakia salama.

Sendiga alibainisha hayo jana wakati akizungumza na wananchi na wanafunzi katika Shule ya Sekondari Chanji iliyopo katika Manispaa ya Sumbawanga.

Akizungumzia walimu wanaojivua maadili, alisema katika shule 19 za sekondari baadhi ya walimu wanatuhumiwa kuwapatia ujauzito wanafunzi wao ambapo watano wameshajifungua.

Aliongeza kuwa baada ya mapimziko ya Sikukuu za mwisho wa mwaka atafanya ziara katika shule hizo ili kubaini hatua walizochukuliwa walimu hao.

“Kwa taarifa zenu ninazo pia nakala za ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) za walimu wakiwasiliana na wanafunzi wao wa kike na jinsi wanavyowahonga. Mkawapatie salamu zangu,” alisema.

Aliwakumbusha wanaume kwamba mtaani kuna wanawake wengi wanaotafuta kuoleawa na hivyo hakuna sababu ya kumfuata mwanafunzi na kuwakumbusha walimu kwamba wao ni wazazi na walezi hivyo ni kinyume cha maadili mwalimu kumtamani mwanafunzi ambaye ni mwanae.

Aliwaonya maofisa elimu sekondari kuacha kuwakingia vifua walimu wanaovunja maadili badala yake wawachukulie hatua za kinidhamu na za kijinai.

Alisema amemwelekeza Mwendesha Mashtaka wa Mkoa amkusanyie mafaili yote ya waliotuhumiwa kubaka na kulawiti watoto ambao mashauri yao yameshindwa kuendelea kwa kukosa ushahidi.

Alisema hiyo ni kutokana na watuhumiwa hao kumalizana na wazazi au walezi wa watoto nje ya mahakama na kwamba kwake mashauri hayo hayajaisha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti CCM Mkoa wa Rukwa, Silafu Maufi aliitaka jamii iwe na hofu ya Mungu, ijiepushe na visa vya ukatili wa kijinsia kwa kumgeukia Mungu.

Habari Zifananazo

Back to top button