TIMU za ABC, JKT na Pazi zimeanza vyema hatua ya kuisaka nusu fainali ya ligi ya mkoa wa Dar es Salaam baada ya kufanya vyema katika mchezo wa kwanza wa robo fainali mwishoni mwa wiki iliyopita.
ABC ilicheza na Outsiders na kushinda pointi 86-78 katika mchezo wenye ushindani. Aidha, JKT ilishinda dhidi ya Oilers kwa pointi 84-68 huku Pazi ikiwachapa VBC kwa pointi 72-41 michezo hiyo ikichezwa kwenye uwanja wa Don Bosco Oysterbay Ijumaa.
Kwa mujibu wa mhamasishaji wa kikapu Justine Kessy, timu zinatakiwa kucheza michezo mitatu na zitakazofuzu zitaingia hatua ya nusu fainali. Timu hizo zilizoshinda zinahitaji ushindi wa mchezo mmoja kila moja kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele. Timu hizo zilitarajiwa kurudiana mchezo mwingine jana kujua nani atakuwa na nafasi ya kusonga mbele hatua inayofuata.
Kwa upande wa wanawake timu zilizoingia nusu fainali ni Vijana Queens na Jeshi Stars ambao watacheza Jumamosi ijayo sawa na JKT Stars itakayocheza na Ukonga Queens ili kutafuta washindi wawili watakaoingia fainali.