ABDUL JUMA : Kinda anayetamba na Zahanati ya Kijiji

Ndiye mtunzi wa Saluni ya Mama Kimbo, Kombolela

 KAMA umewahi kuzifuatilia tamthiliya za Saluni ya Mama Kimbo na Kombolela, bila shaka hujaacha kufuatilia tamthiliya ya Zahanati ya Kijiji katika king’amuzi cha Azam kwenye chaneli yake ya Sinema zetu.

Mtunzi wa tamthiliya hizi ametulia na hadithi zake haziishi hamu, ndio maana nasema kama ulifuatilia tamthiliya zake mbili za mwanzo, huwezi kuacha kufuatilia hii inayoendelea sasa ya Zahanati ya Kijiji.

Anaitwa Abdul Juma, ni kijana mdogo lakini hakuna ubishi kwamba anafanya kazi kubwa kwenye sanaa hiyo.

Tamthiliya ni nyingi siku hizi, lakini hizi za Abdul ni za kipekee kwa sababu hajaingiza usasa kama zilivyo nyingine, kwamba hata kama kuna vipande vya kijijini lakini vya mjini pia vipo.

Watu wako kwenye magari makubwa, wanafanya kazi kwenye ofisi nzuri, wanaishi nyumba nzuri, watoto wao wanasoma shule nzuri, mara wako mezani wanakula, viingereza vingi, ndivyo zilivyozoeleka tamthiliya ama filamu nyingi.

Kwa Abdul si hivyo, amekuwa akitunga tamthiliya zake kama ni watu wa kijijini basi kijijini kweli, kama ni watu wa uswahilini basi uswahilini kweli mwanzo mpaka mwisho na hapo ndipo utamu wa tamthiliya zake ulipo.

Kwa nini hapendi usasa?

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili mkoani Dar es Salaam hivi karibuni, Abdul anasema anafanya hivyo kwa sababu huko ndiko kwenye simulizi nyingi zinazogusa tabaka la chini na la kati.

“Na kiukweli hao ndio wateja wetu na huwa wanafurahi wakiona unawagusa kwa ukubwa na kwa upana ambao ukiwagusa wanafurahi.”

Kwenye Zahanati ya Kijiji kuna visa vingi kila mahali na havichoshi. Umefuatilia maisha ya mama Mwazani (Shamila Ndwangila- maarufu Bi Star) na watoto wake Mwazani (Tishi Abdallah) na Mbwana (Said Zubery maarufu Kimbembe)? Maisha ya Dk Ombeni (Bakary Mizinga) na nesi Mauja (Beatrice Taisamo)?  Abdul amelenga nini kwenye hadithi hiyo.

“Kuna vingi vya kujifunza kwenye hivi vitu, mfano Ombeni na Mauja. Ombeni ni mgonjwa ametoka familia ya kitajiri inayojiweza lakini amekubali kwenda kufanya kazi kijijini, jambo ambalo wengi hawawezi katika asilimia 90 nadhani ni 20 ndio wanaweza kufanya hivyo, tena nyumbani kwao wakiwa wanajiweza, kwa hiyo ameonesha uzalendo mkubwa sana.”

“Moja, nilitaka kutuma ujumbe kwa vijana kwamba popote maisha yanawezekana ni wewe tu jinsi unavyoweza kujitafsiri.

“Lakini alivyofika pale (kijijini) akajikuta ameubwaga moyo kwa mtu ambaye sio rika lake, hafanani naye kwa lolote ni muuguzi wa muda mrefu na mgonjwa… wanasema mtu anaweza akawa mwathirika wa virusi vya Ukimwi lakini anaweza kutengeneza familia, nilikuwa nataka kukazia kwamba hata uwe na magumu kiasi gani lakini maisha yanaendelea.

“Mauja alikuwa mtu aliyekwisha kukata tamaa, alijisusa, hakuna yeyote ambaye angemwambia lolote akamuelewa lakini Ombeni alipokuja akabadilisha kila kitu chake.

“Lakini pia kwenye suala la malezi nimeliibua kwa mapana yake, mfano mama Mwazani, pengine ni mama bora, lakini hana njia sahihi za kuonesha ubora wake, ana watoto wawili mmoja wa kiume na mwingine wa kike. Kwa wa kike tumeona jinsi anavyomchochea aungane na fulani, na aachane na fulani, anataka mwanaye aishi maisha mazuri.

“Maisha mazuri pengine yanaweza kupatikana lakini sio mpaka kwa mwanaume, anaweza kujishughulisha mwenyewe na mambo yakaenda, ana mtoto wa kiume ambaye mpaka katika umri wa miaka 17, 16 hajui kusoma, lakini yuko kwake, anakua akimuona, anaharibika akimuona. Yeye yuko bize anahangaika na ya kijiji, hakuna la kijiji linalopita asilijue, lakini kumbe anavyohangaika na ya mbali, yaliyo karibu yake yanamong’onyoka.”

Anasema kisa cha mama Mwazani ni la kuvunda halina ubani, maana sasa Mbwana anakaribia kufanya mitihani ya kidato cha nne na hajui kusoma. Pengine angekuwa karibu na mtoto angejua mengi na kupata nafasi nzuri kurekebisha.

“Nimetoa ujumbe mkubwa kwenye malezi. Umemuona baba yake, alijitahidi lakini mama alikuwa na nguvu zaidi, unagundua kumbe tunahitaji ushirikiano wa wazazi wote wawili katika malezi, baba na mama, lakini mama ndio uti wa mgongo.

Tamthiliya hiyo imechezwa kwenye Kijiji cha Mwembe togwa, Lindi, ambapo kuna Mtendaji wa Kijiji hicho, Mcdonald Haule na mkewe mwalimu Norinda.

Norinda ni miongoni mwa wanawake wanaonyanyasika na waume zao, akinyimwa uhuru wa kufanya mambo muhimu ya kijamii na kuambulia vipigo, aliwahi kupigwa mpaka kuharibu ujauzito wake aliokuwa mwishoni kujifungua, lakini bado anang’ang’ania ndoa hiyo yenye mateso.

Abdul anasema kwenye kipande hicho cha Mtendaji ni kisa cha kweli alichoamua kukiingiza kwenye tamthiliya hiyo ili kufikisha ujumbe wa ukatili wa kijinsia.

“Mtendaji ni mtu katili. Ukatili wa kijinsia umekuwa mkubwa sana kwa sasa, pengine watu wanaona haya kuzungumza lakini vipo na mimi kwa uchache nimeshuhudia,” anasema.

Anasema wakati anataka kurekodi tamthiliya ya Zahanati ya Kijiji alitafuta kijiji cha kufanyia kipande kimoja (demo) kwa ajili ya kuiuza kupata sehemu itakayokuwa inaoneshwa, akapata kituo kimoja cha afya Kimbiji.

“Mganga mfawidhi wa hiyo zahanati ni mwanamke na ameolewa na mtu mwenye nguvu sana, lakini tulipoegesha tu magari tunashusha kamera yule mwanaume akaona huo ugeni, alipiga simu wilayani Kigamboni na kushitaki kuna uvamizi,” anabainisha.

Anasema baada ya muda yule mganga mfawidhi akapigiwa simu na kuamrishwa awaambie Abdul na kundi lake waondoke.

“Dada alikuwa analia, ilibidi niwasiliane na Mwenyekiti wa eneo hilo kupata msaada maana watu mlishaingia gharama unajua lakini dada akaniambia hawezi kunisaidia maana aliyepiga simu ni mumewe na ni mkali na siku hiyo angekiona. Mwenyekiti akaniambia hawezi kusaidia lolote maana mume wa huyo dada anamfahamu na kwamba  anapitia kwenye mazingira magumu sana…

“Huwezi amini hatujamaliza mazungumzo yule mumewe akaingia anamuuliza unasubiri nini mbona hufungi, fikiria ilikuwa saa saba mchana sijui saa nane, akamwambia funga kituo nakuhitaji nyumbani, yule dada akasema basi jamani mume wangu amekuja kweli akafunga kituo akaondoka,” anasema.

Anasema alibaki na butwaa na kumuuliza mwenyekiti kama kuna zahanati nyingine wanaweza kuitumia, ghafla akapigiwa simu na yule dada (daktari) akimwambia waondoke mumewe anahoji kwanini mpaka sasa bado wapo hapo.

“Kwa hiyo kutoka hapo nikasema kuna haja ya kuzungumzia hivi vitu, watu wanapokwenda vijijini kufanya kazi wanajisusa wanajisahau wao ni kina nani, hawatendei haki elimu yao, kwa hiyo nikaibadilisha ikawa ni mwalimu wa sekondari ambaye anapitia magumu kutoka kwa mtu mwenye nguvu kijijini.”

Kuhusu watu maarufu na wasanii wa muziki kuingia kwenye tamthiliya miaka ya karibuni, Abdul anasema huko ndiko kunakolipa.

“Unajua kwenye tamthiliya ni mahali ambapo mtu anaweza kuonekana muda mwingi na pengine kwenye muziki kuna foleni kubwa kwa hiyo anataka muendelezo na ndio tasnia inayotoa mastaa wenye muendelezo.”

Bi star ni msanii mkongwe ambaye amekuwepo kwenye tamthiliya zote tatu za Abdul, kwa nini?

Anasema kazi anayofanya mwanamke huyo sio ya kitoto na katika tamthiliya zake yeye ndio anamuona anafiti kucheza sehemu anazotaka.

“Ilishawahi kutokea yupo kwenye tamthiliya fulani iliyokuwa inarushwa na Azam hivyo sikutakiwa kumtumia sababu haitakiwi mtu mmoja kuonekana kwenye tamthiliya nyingi zinazorushwa na kituo hicho, huwezi amini nililazimika kusubiri ile tamthiliya iishe ndio nimtumie,” anasema.

Serikali

Anasema serikali na sanaa haviko karibu anatamani viwe karibu zaidi kwani wasanii wanapitia magumu.

“Mioyo yetu inavuja damu, kodi kubwa… lakini tuna thamani sana kwa tunachokifanya, nashauri tu izidishe ukaribu,” anasema Abdul ambaye kitaaluma ni mwalimu wa lugha aliyewahi kufundisha Shule ya Sekondari Tusiime kwa miaka mitatu.

Mwisho

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button