Abiria afariki akisubiri ndege

MTU mmoja amekutwa amefariki dunia wakati akisubiri kusafiri kwa ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) uliopo Nairobi.

Taarifa zinasena polisi wanaendelea kuchunguza kifo cha abiria huyo ambaye mwili wake ulipatikana kwenye chumba cha abiria kusubiria ndege katika uwanja huo.

Kwa mujibu wa polisi, abiria huyo mwenye umri wa miaka 43, alielekea Mombasa Jumamosi, Aprili 8 usiku na alikuwa ameingia tayari kwa kupanda ndege, lakini hakupanda ndege muda ulipowadia na abiria kutakiwa kufanya hivyo.

Ilisemekana kuwa, maofisa wa shirika la ndege la Jambojet walikuwa wakiita jina lake mara kadhaa wakimtaka apande, ili ndege iondoke lakini hawakufanikiwa kwa kuwa hakutokea.

“Abiria huyo alikuwa kwenye moja ya viti katika chumba cha kusubiri na alifia hapo akiwa ameshikilia begi la kusafiria,” mmoja wa maofisa hao alisema na kuongeza kuwa, sababu ya kifo chake haijabainika.

Hata hivyo, walisema alibainika akiwa ametulia kwenye kiti na maofisa wa afya wa shirika hilo la ndege waliitwa kumhudumia kabla ya kutangaza kuwa amefariki dunia.

Polisi bado hawajabaini chanzo cha kifo lakin walikuwa wameiarifu familia ya marehemu na mwili wake ulihamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ukisubiri uchunguzi zaidi.

Habari Zifananazo

Back to top button