MKUU wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi (pichani) amepongeza wananchi wanaotoa ushirikiano kwa makarani wa sensa ya watu na makazi.
Makilagi alisema hayo wakati akiwa katika bandari ya Mwanza North mkoani Mwanza ambako abiria waliokuwa kwenye meli ya New MV Victoria wakiwa wanatoka Kagera kwenda Mwanza walihesabiwa.
Makilagi alisema pia walihesabu watoto wa mitaani, watu kwenye hoteli na nyumba za kulala wageni na wananchi waliokuwa kituo cha mabasi cha Nyegezi.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala alisema sensa katika wilaya hiyo inaendelea vyema na makarani wapo kazini.
Maofisa watendaji wa kata za Sengerema waliwapongeza wananchi wa kata hizo kwa kujitokeza kuhesabiwa.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chifunfu, Elikana Ndiganya alisema: “Zoezi hili ni zuri sana na wakazi wa kata yetu wanafurahia sana zoezi.Pia ushirikiano ni mkubwa sana wananchi wanaonyesha kwa makarani katika maeneo mbalimbali.’’
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Nyamplukano, Kepha Chima alisema sensa katika kata hiyo walitembelea nyumba 25 za kulala wageni katika kata yao ili kuchukua taarifa za waliolala humo.
Mkufunzi wa sensa ngazi ya mkoa, Joanitha Rutizibwa alisema katika Kata ya Nyampulukano kuna makarani kama 15 bado hawajalipwa kutokana na akaunti za makarani hao kuwa na matatizo ya kutowekewa fedha muda mrefu.
Alisema wanatarajia malipo ya makarani hayo yangetolewa kuanzia jana. Mtendaji wa Kata ya Nyamazugo, Martha Mahenge alisema zoezi la sensa linaendelea vyema na kata yake ina makarani 29 na wasimamizi wawili