MKAZI wa Kijiji cha Kibwela, Kata ya Nyawilimilwa wilayani Geita, Mathayo Gote, ameadhibiwa kwa kuchapwa viboko na kutozwa faini ya Sh 200,000, baada ya kufumaniwa na mke wa mpangaji wake.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kabwela, Simeo Sanane ameeleza kwamba adhabu hiyo imekuja baada ya kuthibitishwa mtuhumiwa alikamatwa ugoni.
“Amekamatwa ugoni, na hatimaye akawa amefikishwa ofisi ya kijiji, na sisi ofisi ya kijiji tuna utaratibu wetu ni kwamba tunafuata taratibu zetu za nzengo tukalipeleka kwa jamii,” amesema.
Amesema adhabu hiyo inakuja baada ya kujiridhisha na upelelezi kuonesha mzee huyo amefanya kitendo cha aina hiyo, mara ya tatu sasa amekamatwa ugoni akiwa na wake za watu.
Naye mpangaji, Emmanuel Ndalawa amesema yeye ana wake wawili na mzee mwenye nyumba alimfumania akiwa na mke mdogo.
“Baada ya kuwa na wanawake wawili, ndipo nilipomuona mzee Gote (mwenye nyumba) nikaanza kuona amekuwa na mazoea na mke mdogo, nikaona mpaka na hela akawa anatoa.
“Nikampiga mke wangu nikamuuliza, kwa nini hii hela umepewa na huyu mzee, sikuwa na makusudio ya kumpiga mzee wetu, sikuwa na nia ya kumpiga kabisa, ikabidi nimuonye tu.
“Kwamba mzee sikukusudia kumpiga mke wangu, ila nimempiga tu kwa sababu ya hili tukio ulilolifanya wewe mwenyewe, sasa hebu naomba sasa uache hii tabia, uache.
“Kwa sababu mimi ninatoka ndani nakuita baba, wanangu wanatoka ndani wanakuita babu, unakuja hapa unapikiwa chakula kama kawaida, tunaishi kama kawaida,” amesema akieleezea namna alivyokuwa akimuasa.
Amesema pamoja na angalizo hilo, lakini ilishangaza usiku wa Machi 22, 2024 wakati akiwa anaenda msalani alimshuhudia mwenye nyumba akihama chumba kwenda chumba cha mke mdogo.
“Ndipo nikamfuata mpaka ndani, nikamkuta akiwa ndani, akiwa akiwa amevalia kaptura tu, ikiwa ni majira ya saa nne usiku,” amesema mpangaji huyo.
Naye mkazi wa Kijiji cha Kabwela, Sharifah Thomas amedai wameshangazwa na tabia chafu za mzee huyo, kwani matendo yake hayaendani na umri wake, hivyo adhabu hiyo ni fundisho kwake.