NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Utumishi Deogratias Ndejembi amewataka Watumishi mkoani Simiyu kujituma na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Aidha, amewataka kutimiza majukumu yao na kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati katika kuwahudumia wananchi ili kufikia lengo la asilimia 70 la utekelezaji wa miradi inayoratibiwa na Serikali kupitia mradi wa Kunusuru Kaya Maskini TASAF mkoani Simiyu
Ndejembi amekemea pia tabia ya baadhi ya Watumishi kutotimiza wajibu wao wa kuhudumia wananchi na kujiingiza katika shughuli zao binafsi ambazo hazilengi kutekeleza mipango ya Seriakli katika kuwahudumia Wananchi.
“Serikali haitafumbia macho watumishi wa umma wanaotumia muda na gharama za serikali kufanya shughuli zao binafsi za kujiingizia kipato badala ya kutekeleza majukumu ya serikali ya kuwahudumiwa wananchi.”Amesema
Amesema serikali haizuii watu kufanya biashara bali shughuli hiyo binafsi anayojihusisha nayo isiingiliane na muda wa kazi za serikali na kutumia gharama ama vifaa vya serikali kwa manufaa binafsi.
“Kila mmoja katika eneo lake asifanye kazi kwa mazoea, ajitume na kujiuliza swali yuko mahali hapo kwa ajili ya nini, ni kuwatumikia wananchi, tusitumie muda wa serikali katika kufanya shughuli zetu binafsi, kila mmoja ajiulize yuko nafasi hiyo kwa ajili ya nini? Uko mahali pale kwa ajili ya kuongeza tija na kuwahudumia wananchi kwa sababu tuko mahali hapo kwa ajili ya kutoa huduma,” alisema.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt Yahaya Nawanda alimuhakikishia Ndejembi kuwa Mkoa utaendelea kusimamia watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao waliyopangiwa na Serikali ili kuongeza tija katika utendaji wa serikali katika kuwahudumia wananchi.
Kuhusiana na miradi ya Tasaf, Nawanda alisema alishakaa na Wakuu wa Wilaya na miradi hiyo kwa sasa ipo katika asilimia 70 za utekelezaji na kuahidi ndani ya mwezi mmoja itakuwa imekamilika, kama walivyofanya katika miradi ya UVICO.