ACT wasifu utendaji wa Majaliwa

KIGOMA: CHAMA cha ACT Wazalendo Mkoa Kigoma kimepongeza hatua ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuunda tume na kamati mbalimbali kufuatilia tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za serikali kwenye hamashauri mbalimbali nchini ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Kigoma Cinema Mjini viongozi wa chama hicho walisema kazi inayofanywa na Waziri Majaliwa haina budi kuungwa mkono na Watanzania wote.

Akizungumzia kwenye mkutano huo aliyekuwa diwani wa kata ya Kitongoni, Maulid Kacheche alisema kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Majaliwa wito wake kwa serikali kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Naye Hussein Kalyango aliyekuwa diwani wa kata ya Kigoma Mjini alisema kuwa Waziri Mkuu amefanya kazi nzuri ya kuunda tume kwa ajili ya kuchunguza tuhuma za ubadhirifu wa Sh milioni 500 Manispaa ya Kigoma Ujiji na tayari watumishi wameanza kuhojiwa na kwamba isiishie kuwahoji bali hatua za kisheria zinapaswa kuchukuliwa.

Pamoja na hilo Kalyango alisema kuwa wao kama madiwani waliomaliza muda wao wana taarifa za tuhuma nyingine za fedha zaidi ya Sh milioni 400 ambazo matumizi yake hayajulikani na hivyo kuomba Waziri Mkuu ajumuishe na hizo kwa tume aliyounda kuchunguza tuhuma za ubadhirifu kwenye manispaa ya Kigoma Ujiji.

Diwani mwingine wa chama hicho, Tatu Amani pamoja na pongezi kwa Waziri Mkuu Majaliwa kwa kazi nzuri anayofanya kuunda tume kuchunguza tuhuma za ubadhirifu amemtaka pia kuunda tume kuchunguza uuzwaji holela maeneo ya wazi kunakofanywa na watendaji wa idara ya ardhi ya halmashauri hiyo jambo ambalo limeleta migogoro mikubwa baina ya serikali na Wananchi.

Habari Zifananazo

Back to top button