ACT-Wazalendo yaja na maazimio saba kutatua ‘dhiki’ ya machinga

ACT-Wazalendo yaja na maazimio saba kutatua ‘dhiki’ ya machinga

HALMASHAURI Kuu ya chama cha ACT-Wazalendo imepitisha maazimio saba ikiwemo sera ya wamachinga inayolenga kutatua madhila na changamoto zinazowakabili wamachinga na hatua za kisera zinazopaswa kuchukuliwa kukabiliana nazo.

Aidha, chama hicho kimeeleza kujizatiti katika kujiendesha kisasa kupitia mfumo wa ACT kiganjani na kutoa maelekezo kwa wanachama wake kuendelea kujiimarisha katika utumiaji wa njia za kidijiti katika uendeshaji wa chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu Dar es Salaam, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Janeth Rithe alisema halmashauri kuu imeelekeza sekretarieti ya chama hicho kupanga uzinduzi wa sera inayohusu wamachinga.

Advertisement

“Halmashauri Kuu imeagiza kamati ya wasemaji wa kisekta kupaza sauti juu ya maeneo mahususi ya kukithiri kwa tozo za serikali, uvunjifu wa haki za binadamu magerezani, changamoto za bima ya afya, umuhimu wa hifadhi ya jamii na mageuzi katika Jeshi la Polisi,” alisema.

Aliongeza kuwa halmashauri hiyo imeelekeza kufanyika kwa uzinduzi wa ofisi ya makao makuu ya chama hicho iliyopo Magomeni, Dar es Salaam ambayo jengo lake limepewa jina la aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kwa lengo la kumuenzi.

Pia alisema halmashauri kuu imepitisha ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama kwa ngazi za matawi, kata, majimbo, mikoa na taifa utakaofanyika kuanzia Machi 2023 hadi Machi 2024.

“Halmashauri kuu imepitisha azimio la kuundwa kwa kitengo cha kusimamia uwajibikaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambacho kitakuwa na majukumu ya kufuatilia kwa karibu uwajibikaji wa serikali na kutoa sera mbadala,” alisisitiza.

Rithe alisema halmashauri hiyo imeelekeza ujenzi wa chama kwa kina kwenye mikoa ya Magharibi (Pwani na Kusini) na mikoa yote ya Zanzibar.

“Mwenyekiti wa chama taifa, Juma Duni Haji ameidhinisha uteuzi wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ambao ni Ally Saleh, Mkunga Sadalla, Suleiman Bungara (Bwege), Nyangaki Shilungushela, Rehema Haji na Pendo Manyanya. Wajumbe wa Kamati ya Maadili taifa ni Ussi Haji (Mwenyekiti) na Juma Khamis Juma (Mjumbe) na Naibu Katibu Ngome ya Vijana Zanzibar ni Mohamed Khamis Bussara,” alifafanua.

 

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *