Adai kuponzwa na mwanamke aliyekutana naye Mlimani City

MSHITAKIWA Bogias Augustine na wenzake wawili wanakabiliwa na mashitaka matatu ikiwemo unyang’anyi kwa kutumia silaha na wizi.

Hata hivyo, Augustine amedai kuwa hakufanya makosa hayo bali alisingiziwa baada ya kuhusishwa kuwa na mahusiano na mwanamke aliyekutana naye Mlimani City.

Mshitakiwa huyo alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ferdnadri Kiwonde wakati akitoa utetezi wake.

Agustino alidai kuwa anaamini alifanyiwa utaratibu wa kukamatwa na mlalamikaji kwani askari waliohusika kumkamata hawakutoa taarifa ya ukamatwaji wake wala hakukuta mashitaka yoyote kituoni.

“Nakumbuka kuna siku nikiwa Mlimani City nilikutana na mwanamke aliyedai ananifananisha na tukabadilishana namba wakati tumesimama alitokea mwanaume mmoja ambaye alimwangalia kwa ghadhabu na kumuamuru mwanamke huyo waondoke,” alidai Agustino.

Alidai kuwa Februari 18, 2022 akiwa nyumbani kwake walifika askari na kumkamata na kufanya upekuzi ndani ya nyumba yake na kumchukua kumpeleka Kituo cha Polisi Kijitonyama.

Alidai kuwa alikaa kituoni hapo hadi Februari 23, 2022 siku hiyo alikuja askari na kumtaka waende Kituo cha Polisi Oysterbay na walipofika walikuja wanaume wanne ambao kati yao alimtambua mmoja wao kuwa ndiye aliyekutana naye Mlimani City, wakati akizungumza na mwanamke huyo na askari huyo alimwambia atamshikisha adabu.

Agustino alidai kuwa baada ya hapo alirudishwa Kituo cha Polisi Kijitonyama hadi Machi 23, 2022 alipofikishwa mahakamani hapo na kuunganishwa na watu wawili ambao walisomewa mashitaka kwa pamoja.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka inadaiwa kuwa Januari 11, 2022 mshitakiwa Augustine akiwa Hoteli ya Denfrance iliyopo Sinza, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam aliiba kifaa cha sauti pamoja na simu janja aina ya Iphone 11 pro max vyenye thamani ya Sh 2,280,000 na fedha taslimu Sh 200,000, mali za Hunaina Salehe na kumtishia kwa kisu ili abaki na mali hizo.

Katika mashitaka ya pili inadaiwa mshitakiwa huyo pia tarehe hiyo hiyo na katika eneo hilo alimpa dawa za kumlevya Hunaina Salehe.

Katika mashitaka ya tatu inadaiwa kuwa Ally Kibuga na Abdallah Mmangi katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2022 katika Mkoa wa Dar es Salaam wakishirikiana walipokea simu ya wizi aina ya Iphone 11 pro max yenye thamani ya Sh 2,280,000 huku wakijua kuwa simu hiyo ni ya wizi.

 

Habari Zifananazo

Back to top button