Adai ukeketaji mpya umeibuka K’njaro

UKEKETAJI mpya maarufu  kwa jina la antena umeibuka mkoani Kilimanjaro ambapo hufanyiwa watoto wadogo.

Akizungumzia hali hiyo ambayo anadai imeibuka miongoni mwa jamii ya wakazi wa Kilimanjaro, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la GAESO mkoani humo, ambaye pia ni  Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Hai, Happiness Eliufoo, amesema baadhi ya jamii wanaendeleza utamaduni huo uliopitwa na wakati na kusababisha vifo vya watoto na wengine kubaki na makovu ya kudumu.

“Wilaya ya Hai sio kisiwa; makabila yetu ya Wachaga, Wameru na Wamasai  nao wanafanya ukeketaji na ukeketaji ulioko huku kwetu ni ule unaitwa antenna.

” Tunaiomba serikali yetu kupitia upya sheria ya ukeketaji na itoe adhabu kali ukiachana na hii adhabu ya sasa,” amesema.

Amesema, jamii inakuja na mbinu mpya kila kukicha kuhusu ukeketaji na ikiwa hatua stahiki hazitachukuliwa kundi la watoto wa kike watafanyiwa ukatili wa kutisha, hivyo elimu inapaswa kuendelea kutolewa kwa jamii.

“Hapa kwetu mara nyingi kuna ukeketaji uliovuka kijiji, unakuta mtu anatoka Sanya Station anakwenda kukeketwa katika Kijiji cha Munge na zaidi tuko jirani na nchi ya Kenya, ambapo unakuta hizi jamii za kifugaji wanakwenda kukeketwa kule kwa wenzetu; hatupo salama tunahitaji elimu na mbinu zaidi ili kukomesha jambo hili,”amesema Happy.

Akizungumza kuhusu hali ya ukeketaji kwa Wilaya ya Hai, Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa unafanyika ukatili wa aina yake kwani hawafanyi tena sherehe.

“Hai wanafanya ukeketaji kwa staili ya aina yake na hii ni pale ambapo mtoto anapozaliwa,  kwa kuwa tunazo hospitali na vituo vya afya na mama amejifungulia mle,  pindi akirudi tu nyumbani anakuja ngariba na kumkeketa kichanga huyo na kama utakuwa unasubiri wafanye sherehe ndio uone wamekeketa huwezi ona haya matukio maana mbinu zilishabadilika,” anasema.

Anasema  ukeketaji ni ukiukwaji wa haki za binadamu lakini unaathiri afya ya kimwili na kiakili kwa mamilioni ya wasichana na wanawake.

“Ukeketaji ni ishara tosha ya  ukosefu wa usawa wa kijinsia uliokita mizizi katika mifumo ya jamii,kiuchumi na kisiasa na ni ukatili wa haki za binadamu na ukatili mkubwa dhidi ya wanawake,” amesema Happy.

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button