Adaiwa kufa kwa kunywa pombe bila kula

MHUDUMU wa baa ya Nyemo, Asia Eliya (24) amefariki dunia kwa madai ya kunywa pombe kupita kiasi bila ya kula chakula.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Picha ya Ndege, Joseph Zambo alisema kuwa Asia alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali.

Zambo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 8, mwaka huu majira ya alfajiri nyuma ya baa kwenye migomba jirani na alipokuwa akifanyia kazi.

“Nilipigiwa simu kuwa kuna mwili wa mtu aliyekufa ilibidi niende na nilipofika niliambiwa mwili umechukuliwa na polisi kupelekwa Tumbi ambapo alikuwa hajafa na alifia njiani,” alisema.

Alisema kuwa wafanyakazi wenzake walisema kuwa siku hiyo Asia alikunywa sana pombe kabla ya umauti kumkuta.

“Alichunguzwa lakini hakukutwa na jeraha lolote wala kuumia popote, hali ambayo inaonesha kuwa inawezekana pombe ndiyo ilisababisha kifo hicho,” alisema Zambo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo alikiri kutokea kwa tukio hilo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button