Adaiwa kufia kwa Mchungaji akiombewa

BINTI aitwaye Consolata Pius (16) anadaiwa kufariki dunia, wakati akiwa nyumbani kwa mchungaji akifanyiwa maombi.

Akizungumzia tukio hilo baba mzazi wa mtoto huyo, Charles Pius amedai mtoto wake amekua akisumbuliwa na maradhi ambayo hata baada ya kumpeleka hospitali hayakuweza kutambulika, ndipo mchungaji alipoomba kumchukua kwa ajili ya kumfanyia maombi.

Amedai siku ya kwanza toka mchungaji huyo wa kanisa la kilokole amchukue alilala nyumbani kwake na siku ya pili ndipo umauti ulipomkuta.

“Mtoto alikua anasumbuliwa na vidonda visivyouma mdomoni, anapiga mswaki lakini haviumi, damu inatoka masikioni lakini ukimuuliza anasema hayaumi, damu inatoka puani ukimuuliza anasema haviumi kwa kweli huo ugonjwa ulituchanganya hata sisi,” amedai baba wa mtoto huyo.

Kwa upande wao baadhi ya majirani wanadai walichanganyikiwa kuona mtoto huyo anatapika damu, ndipo walipochukua uamuzi wa kumpigia mchungaji kwa lengo la kwenda nyumbani kumuombea.

“Mimi nilipiga simu kwa wachungaji, hao ambao tunasali nao wakaja wakamuombea, bibi yake akasema mchukueni muende naye hukohuko, tutakua tunakuja tunamuona wakamchukua, wakakaa naye kule ndani ya siku mbili hali ikabadilika hadi alipokutwa na umauti,”amesema jirani aliyejitambulisha kwa jina moja la Joyce.

“Huyu binti ni jirani yangu na alikua Dar es salaam anafanya kazi, alipokuja hakukaa siku nyingi kama siku tatu hivi akaja kwangu akasema, babu mimi madonda yamenitoka mdomoni, wala hayaumi hayawashi naomba unioneshe dawa ya madonda nikamwambia sielewi msaada ni kwenda zahanati ukapate ushauri.

“Hali ilizidi ikabidi aende zahanati¬† kwenye vipimo wakasema anaumwa malaria na U.T.I, wakampa dawa wakampa na rufaa kwenda hospitali kubwa alipofika akapewa kitanda ikaonekana damu hana ikabidi watu wakajitolee damu na kweli walikwenda baada ya hapo aliruhusiwa akarudi.

“Alikaa siku ya kwanza ya pili ugonjwa tena ukarudi, ndio mchungaji akaja hapa wakamuombea na kumbeba kumpeleka kwake alishinda juzi, jana akafariki,” amesema John Mathias.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkuyuni Kata ya Magamba Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, Getani Chambanenge amekiri kutokea kwa tukio hilo, huku akiwataka wananchi kutolihusisha na imani za kishirikina.

Naye Mtumishi wa Mungu Peter James anaedaiwa kumchukua mtoto huyo, amedai alimchukua kwa lengo la kumsaidia kutokana na mazingira magumu aliyokuwa akiishi.

Amedai alipigiwa simu na familia ya mtoto huyo kwenda nyumbani kumfanyia maombi, baada ya kukuta anaishi kwenye mazingira magumu wao kama kanisa walimchukua kwa ajili ya kumuhudumia ikiwa ni pamoja na kumfanyia maombi.

Habari Zifananazo

Back to top button