POLISI mkoani Arusha, inawashikilia watuhumiwa 38, wanaojihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu, akiwemo dereva mmoja aliyekutwa akisafirisha kilo 390 za mirungi kwenye lori la mafuta.
Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Justine Masejo, alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti .
Alisema operesheni hiyo ilifanyika kuanzia Septemba 5 hadi Septemba 10, 2022 na iliongozwa na Mkuu wa upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha, kwa lengo la kukabiliana na uhalifu, ambao umeanza kutishia amani mkoani hapa.
Kamanda Masejo alisema kuwa Septemba 10 mwaka huu majira ya saa 12:30 asubuhi, katika kata ya Kikwe wilayani Arumeru, Jeshi hilo lilifanikiwa kumkamata, Allen Wilbard Kasamu (49), dereva na mkazi wa Suye jijini Arusha, akiwa anasafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi yenye uzito wa kilo 390.75
Alibainisha kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa akisafirisha mirungi hiyo kwa kutumia gari aina ya Mitsubish Canter– Tanker, ambalo ni maalumu kwa ajili ya kubeba mafuta, ambapo mtuhumiwa alipakia ndani ya tenki la mafuta, ili asijulikane.
Pia amesema katika operesheni hiyo jeshi hilo lilifanikiwa kukamata pikipiki 13 zilizokua zinatumika katika matukio ya uhalifu, gongo lita 8, bangi yenye uzito wa kilo 70 pamoja na laptop 3.
Alisema kuwa hadi sasa Polisi mkoani humo, bado inaendelea na upelelezi, ikiwemo kuwahoji watuhumiwa hao.