‘Adakwa’ kwa kusababisha ajali

MWANZA: JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia, Noel Mwanzwila (34) dereva kwa kosa la kugonga gari lingine na kusababisha majeruhi.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza Wilbrod Mutafungwa amesema kuwa ajali hiyo imetokea Mei.1,2024 majira ya saa 20:40 katika barabara ya Mwanza -Shinyanga eneo la mawe matatu, kata ya Usagara wilayani Misungwi.

“Gari yenye namba za usajili T.669 DEE aina ya Higher Bus iliyokua ikitokea Mwanza kwenda Dar -es-Salaam ikiendeshwa na Noel Manzwila aligongana na gari lenye namba za usajili T.858 DHE aina ya Toyota Hiace inayofanya safari zake kati ya Ngudu-Nyashishi ikiendeshwa na Isaka Salumu Bakari (32) ilipokua ikielekea Nyashishi na kusababisha majeruhi kwa abiria wawili waliokua ndani ya Hiace,” amesema Kamanda Mutafungwa.

“Majeruhi wote walifikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi na baadae kuhamishiwa Hospitali ya Mkoa Sekou-Toure kwa matibabu zaidi ambapo chanzo cha ajili hiyo ni uzembe wa dereva wa gari T.669 DEE aina ya Higher Bus kulipita gari lilikuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari, “amesema Kamanda Mutafungwa.

Pia kamanda Mutafungwa ameongeza kuwa dereva huyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani.

 

Habari Zifananazo

Back to top button