KATIBU Mkuu wa Chama cha ‘Alliance For the Democratic Change’ (ADC), Doyo Hassan Doyo amesema kitendo cha Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuitisha mkutano na vyama vya siasa kinapaswa kupongezwa kwa kuwa kinaimarisha afya katika siasa nchini.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Doyo amesema hatua hiyo ya Rais Samia, ni wazi imeonesha dhamira yake ya kweli kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika siasa, hususani kwa vyama vya upinzani na kwamba kwa kuliona hilo ameona ni vyema kukaa nao pamoja na kuzungumza.
Rais Samia kesho anatarajia kukutana na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa katika mkutano unaotarajiwa kufanyika Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam, mkutano ambao baadhi ya wadau wa masuala ya siasa nchini akiwemo Katibu huyo wa ADC wamesema unaashiria jambo jema ikizingatiwa ni mwanzo tu wa mwaka.
“Ukweli binafsi nimefarijika na hatua ya Rais Samia kuitisha mkutano huu mapema kabisa kwa mwaka, hizi ni dalili tosha kuwa lengo ni kuona tunakuwa na mipango ya uhakika kwa kila mmoja wetu katika siasa, sisi kama chama cha siasa ambao pia tutashiriki mkutano huo tunaipongeza hatua hii,” alisema Doyo.

Amesema ADC watahakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kuitikia wito huo na kwenda kutoa mchango wa mawazo yao pale watakapopewa nafasi, lengo ni kuona hali ya kisiasa nchini inaimarika kama ambavyo imeanza kujionesha hivi karibuni tangu Rais Samia ashike madaraka ya kuongoza nchi.
Amewataka viongozi na wanachama wa vyama vingine vya siasa kuhakikisha kwa nafasi zao pia wanajitokeza na kwenda kushiriki mkutano huo na kuwasilisha yote waliyonayo hatua itakayosaidia wapate majibu juu ya yale wanayaona hayastahili au yaboreshwe ndani ya siasa.