ADFA, Mega FM waandaa Arusha Super Cup

CHAMA Cha Soka Wilaya ya Arusha (ADFA) kwa kushirikiana na Mega FM Redio wameandaa mashindano yatakajulikana kwa jina la ‘’Mega FM Arusha Super Cup’’ ambapo mshindi atajinyakulia zawadi ya 1,000,000.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Arusha ,Makamu Mwenyekiti wa ADFA,Isabela Mwampamba alisema kuwa lengo la kuanzishwa kwa mashindano hayo ni kutaka mchezo wa soka katika Jiji la Arusha uchezwe kwa umri wa aina yote ili kila mpenda soka aweze kupata burudani ndani ya Jiji hilo.

Mwampamba alisema na kuwataka wenye kampuni na taasisi binafsi kuiga mfano wa uongozi wa Mega FM kwa kudhamini mashindano hayo kwani lengo ni kukuza soka katika Jiji la Arusha na viunga vyake.

Advertisement

Alisema mshindi wa pili katika mashindano hayo atajinyakulia zawadi ya shilingi 500,000 na timu zote zitazoingia hatua ya robo fainali zitapewa seti moja ya jezi kutoka kwa mdhamini Mega Fm.

Makamu alisema kuwa katika mashindano hayo kutakuwa na zawadi mbalimbali ikiwemo ya mfungaji bora,timu yenye nidhamu na mwamuzi bora  wa mashindano pamoja na waandishi bora katika vitengo mbalimbali vya habari.

Naye mwakilishi wa vilabu,Philimini Mwansasu aliwataka viongozi wa vilabu vyote katika Jiji la Arusha vilivyosajiliwa na visivyosajiliwa kuhakikisha zinashiriki mashindano hayo yenye lengo la kuwapa bize vijana kujikita katika soka na kuacha kushiriki mambo ya hovyo kwa jamii inayowazunguka.

‘’Tunataka soka lichezwe katika Jiji la Arusha kwa umri wote ili kuandaa timu bora kwa wakazi wa Jiji hilo kwa hapo baadae’’alisema Mwansasu

Naye Katibu Mkuu wa ADFA,Fredrick Lyimo maarufu kwa jina la Deco alisema baada ya Shirikisho la Soka Nchini{TFF} baada ya kuweka vigezo vya umri katika ligi daraja la nne ngazi ya wilaya wachezaji wanaoshiriki kuwa na umri chini ya miaka 20 sasa wamekuja na mashindnao hayo ili Jiji liwe bize katika mashindano ya soka kwa muda wote.

Deco alisema soka ni burudani na burudani ya soka inapaswa kuratibiwa na ADFA kwani ndio wenye vilabu katika wilaya hivyo kuanzisha mashindano hayo kuna lengo la kutaka vijana kujikita katika soka na sio vinginevyo.