“Afrika Mashariki waige kwa waliofanikiwa”

NCHI za Afrika Mashariki zinaweza kujifunza kutoka kwenye nchi nyingine zilizofanikiwa kwa kuiga ujuzi wanaoutumia.

Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Gatsby, inayofanya kazi katika nchi nne za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, Uganda, Kenya na Rwanda, Samweli Kilua amesema hayo alipozungumza kuhusu Kongamano la 27 la mwaka katika masuala ya Utafiti lililoandaliwa na Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini Tanzania (Repoa).

“Nchi za Afrika Mashariki zinaweza kujifunza kutoka kwenye nchi nyingine zilizofanikiwa kwa hiyo moja wapo wa kazi nyingine ni kufanya tafiti, kuchambua na kujaribu kushirikisha wengine ili waweze kuona kwamba wenzao wengine wamefanyaje sehemu nyingine,” amesema.

Advertisement

Amesema katika nchi za Afrika Mashariki na ulimwengu mzima kumekuwepo na tatizo la uhaba wa kazi ndio sababu wanaegemea kwenye suala la uchumi ili uwe imara zaidi, shirikishi zaidi na ambao unatekeleza kazi nyingi zaidi.

Amesema ni muhimu kwa nchi yoyote kutoa kipaumbele kwenye sekta zenye fursa kubwa ya kukua na kuchangia katika uchumi wan chi, pamoja na kuweza kutengeneza ajira nyingi.

Amesema wanashirikiana na Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini Tanzania (Repoa), kwa kuwa katika kongamano hilo watatoa mada inayozungumzia umuhimu wa sekta katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari amesema katika kongamano hilo watazindua program kubwa ya utafiti wa miaka mitano ambayo itajikita kwenye eneo la namna ya kubadilisha muundo wa uchumi wa nchi ya Tanzania.

“Pia utaangalia vyanzo vya ukuaji wan chi, ukuaji wa uchumi, mabadiliko lakini namna gani ya kuongeza tija katika uzalishaji kwenye sekta kubwa za uzalishaji na jinsi gani sekta hizo zinavyoweza kuingiliana, sekta ya kilimo na sekta ya viwanda.

“Kwa mfano sekta ya uchukuzi inaweza kuingiliana vipi ili kuweza kuhakikisha zote zinaondoa changamoto ambazo zinazuia ukuaji wa uchumi,” amesema.

Amesema pia yapo maendeleo kama mabadiliko ya muundo wa idadi ya watu, “ukiangalia Tanzania asilimia 60 ya wananchi wake wana umri chini ya miaka 24 sasa hii ina maana gani kwa uchumi ina maana gani kwa soko la ajira, ina maana gani katika tija ya uzalishaji , ina maana gani katika teknolojia ni jinsi gani Tanzania inaweza ikatambua teknolojia,”.

2 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *