Afrika nyuma ya Morocco leo

MOROCCO leo inakuwa timu ya kwanza ya Afrika kucheza nusu fainali za Kombe la Dunia itakapomenyana na mabingwa watetezi, Ufaransa kwenye Uwanja wa Al Bayt mjini hapa.

Nusu fainali ya kwanza ilitarajiwa kuchezwa jana usiku ambapo Agentina ikiongozwa na nyota wake, Lionel Messi ilikuwa uwanjani dhidi ya Croatia chini ya ‘msumbufu’, Luka Modric.

Aidha, katika mechi hiyo, Ufaransa inawania kuwa timu ya kwanza tangu Brazil mwaka 1962 kushinda Kombe la Dunia mara mbili mfululizo.

Katika mechi ya leo, Olivier Giroud aliyefunga bao la ushindi kwa Ufaransa katika mechi ya robo fainali dhidi ya England Jumamosi iliyopita anatarajia kuendeleza makali yake.

Ufaransa huenda isiwe na makali kama ilivyokuwa kwenye michuano ya mwaka 2018 Urusi, lakini ipo nusu fainali na inaonekana kuwa na uwezo wa kucheza fainali kutetea taji lake.

Pamoja na kuwa majeruhi kwa Karim Benzema, Paul Pogba, N’Golo Kante, Christopher Nkunku na Presnel Kimpembe, Kocha mkuu, Didier Deschamps ameunda kikosi kingine ambacho hakimuangushi.

Ufaransa haijawahi kufungwa na Morocco katika mechi zote tano walizokutana, wakishinda tatu na kutoa sare mbili.

Les Bleus inacheza nusu fainali yake ya saba ya Kombe la Dunia, ikishinda mechi zote tatu zilizopita katika hatua hii.

Mchezaji wa Ufaransa, Antoine Griezmann amehusishwa kwenye mabao manane katika mechi nane za Kombe la Dunia alizoanza akifunga mabao matatu na kutoa pasi za bao tano.

Morocco inaongozwa na kocha Walid Regragui aliyeteuliwa si zaidi ya miezi mitatu kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia.

Kwa lolote litakalotokea dhidi ya Ufaransa leo, kikosi hiki cha Morocco kitakumbukwa kama mashujaa. Ni taifa la kwanza la Afrika kucheza nusu fainali ya michuano hii.

Habari Zifananazo

Back to top button