Afungwa jela kwa kukata kiganja cha bosi

MKAZI wa Ludewa mkoani Njombe, Baraka Luoga (20) amehukumiwa kifungo cha miaka minne jela kwa kosa la kumjeruhi kwa kumkata kiganja cha mkono bosi wake, Patrick Mdege (35), kwa madai ya Sh 65,000.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Ludewa, Isaac Ayengo, Mwendesha Mashtaka, Angelo Marco ilielezwa kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 25, mwaka jana.

Alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo wakiwa mashambani baada ya kupishana kauli wakati wakieleweshana juu ya malipo ya fedha hizo.

Ilielezwa kuwa baada ya kusomewa shitaka lake kwa mara ya kwanza, mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo.

Mwendesha mashtaka, Marco aliiomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa kifungu cha sheria ili iwe fundisho kwa wengine.

Hakimu Ayengo alitoa hukumu hiyo kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 225 sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka mwaka jana.

Mshitakiwa aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwani ni kosa lake la kwanza na ana wazazi walio wazee wanao mtegemea.

Habari Zifananazo

Back to top button