MKAZI wa Mtaa wa Ghana Kata ya Kiloleni, Manispaa ya Tabora, amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wa miaka tisa.
Adhabu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Tabora, John Mdoe baada ya kuridhika na ushahidi usioacha shaka uliotolewa na upande wa mashitaka.
Hakimu Mdoe alisema ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi wanane wa upande wa mashitaka akiwamo mtoto aliyefanyiwa kitendo na wa daktari, ulithibitisha pasipo shaka kwamba mshitakiwa ndiye alitenda kosa hilo Juni 15, 2021.
Awali, upande wa Jamhuri ukiongozwa na wakili Jaines Kihwelo ulidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Juni 15, 2021 katika Mtaa wa Ghana, Kata ya Kiloleni mjini Tabora.
Ilidaiwa kuwa siku hiyo mlalamikaji ambaye jina limehifadhiwa, mwanafunzi mwenye umri wa miaka tisa baada ya kutoka shule majira ya saa 7 mchana alitumwa na bibi yake kwa jirani yake lakini alirejea saa 4 usiku.
Upande wa mashitaka uliongeza kuwa mshitakiwa ndiye aliyemsindikiza nyumbani kwao mtoto huyo na alimdanganya bibi yake kwamba amemkuta njiani ndipo akaamua kumsindikiza kwani ilikuwa ni usiku.
Inadaiwa kuwa shangazi wa mtoto huyo ambaye ni miongoni mwa mashahidi baada ya kumhoji na kumfanyia upekuzi, alikuta sehemu za siri zikiwa zimevimba pamoja na damu iliyoganda.
Chamkoko katika utetezi wake alidai kuwa kulikuwa na kutoelewana baina yake na bibi wa mtoto huyo kwani aliwahi kumtamkia maneno kwamba atampoteza kama ilivyotokea.
Aliiomba mahakama itumie vipimo vya DNA kuthibitisha kosa lake hoja ambayo ilitupiliwa mbali kwa kukosa mashiko ya kisheria.
Akitoa hukumu ya kesi hiyo, Hakimu Mdoe alisema sheria inaelekeza kwamba endapo muathirika ni mtoto chini ya umri wa miaka 10, adhabu kwa mkosaji ni moja ambayo ni kifungo cha maisha jela.