Afungwa jela maisha kwa kulawiti hadharani

Afungwa jela maisha kwa kulawiti hadharani

MAHAKAMA ya Wilaya ya Tabora imemhukumu mkazi wa Kidatu “B” Kata ya Mtendeni mkoani Tabora, Hussein Mashibu (32) kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtu mzima hadharani huku watu wakishuhudia kwa kumtuhumu kuwa ana mahusiano na mke wake.

Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Tabora, Sigwa Mzige alisema mahakama imeona kifungo hicho kwa mshitakiwa kinastahili kwani alifanya unyama usioweza kuvumiliwa na jamii.

Alisema kifungo hicho kitakuwa fundisho kwa mshitakiwa huyo na wengine wenye nia ya kuwadhalilisha watu wengine kutokana na wivu wa mapenzi.

Advertisement

Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Wilaya Tabora, Mzige alisema ushahidi uliotolewa umeonesha hauna shaka yoyote ukilinganisha na ushahidi uliotolewa na mtuhumiwa mwenyewe na daktari ambaye alithibitisha kutokana na vipimo vya aliyelawitiwa kupata michubuko na alipewa dawa ya misuli.

“Mahakama zote nchini zinafanya kazi vizuri kuhakikisha kila mtuhumiwa analetwa hapa kwa makosa mbalimbali kila kosa moja lina adhabu yake,” alisema.

Awali Wakili wa Serikali, Robert Kumwembe aliiambia mahakama hiyo kwamba mshitakiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza anapaswa kupata adhabu hiyo ya kwenda jela maisha.

Wakili huyo aliiambia mahakama hiyo kwamba mtuhumiwa alipatikana na kosa la kumlawiti mtu mzima (jina limehifadhiwa) Januari 30, mwaka jana katika maeneo ya Kidatu ‘B’ mkoani Tabora.

Mtuhumiwa alishitakiwa kwa makosa mawili ya kulawiti na kujeruhi kwa kumpiga na kitu kichwani na kumsababishia jeraha na makosa yote yanakwenda pamoja ikiwemo kulipa faini ya Sh milioni moja.

Mtuhumiwa huyo katika utetezi wake aliiambia mahakama hiyo kuwa alipata tetesi kwamba mtu huyo ana mahusiano na mke wake na siku hiyo alimfumania akiwa na mke wake ndani.

Mtuhumiwa huyo aliiomba mahakama hiyo kuwa impunguzie adhabu hiyo kutokana na kuwa na familia ya watu sita na mke wake kulazwa Hospitali ya Rufaa Kitete kwa ajili ya kujifungua.

Mahakama hiyo ilitupilia mbali ombi la mtuhumiwa huyo kwa kuwa hukumu yake ilikuwa sawa na kosa la kulawiti ambapo adhabu yake ni kifungo cha maisha jela.

/* */