TIMU ya Wizara ya Afya na Benki ya CRDB zimenza vyema Mashindano ya Mei Mosi baada ya kuwafunga wapinzani wao kwa mabao 2-1 kila mmoja katika mchezo wa soka kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa jana.
CRDB wenyewe waliibuka na ushindi huo dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mabao 2-1 yaliyofungwa na Yusuph Ramadhani na Nicodemus Milinga huku TRA bao lake la kufutia machozi lilifungwa na Maximilian Magucho.
Wizara ya Afya wenyewe waliwachapa Wizara ya Kilimo kwa mabao 2-1, mabao ya washindi yalifungwa na Anthony Emmilius na Andrew Jonas wakati lile la Wizara ya Kilimo liliwekwa kimiani na Prosper Ogola.
Nahodha wa Wizara ya Afya, Sadik Lusinga alikiri mchezo ulikuwa mgumu licha ya ushindi walioupata, kwani wapinzani wao walikuwa wazuri.
Timu ya Wizara ya Afya ilikianza kipindi cha pili kwa Kasi kubwa baada ya benchi ya ufundi kufanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji ambao waliongeza nguvu wakiwa na dhamira ya kusawazisha bao hilo na hata kuongeza zaidi.
Kwa upande wake Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Wizara ya Kilimo, Linus Bwegoge alisema licha ya kupoteza mchezo huo wa kwanza katika kundi lao, bado wanayo nafasi ya kujipanga kufanya vyema katika michezo inayofuatia.
Michezo hiyo itaendelea tena leo kwenye viwanja tofauti na katika soka kwenye uwanja wa Jamhuri, timu ya Maliasili itacheza na Uchukuzi,, ambapo mchezo wa pili utakuwa ni kati ya timu ya Ulinzi dhidi ya Hazina .
Kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), timu ya Ushirika itavaana na Mambo ya Nje, na mchezo wa pili ni kati ya Utumishi dhidi ya Tanesco, na kwenye Uwanja wa Chuo cha Ujenzi, timu ya Mawasiliano itamenyana na Afya .
Katika netiboli, kwenye Uwanja wa Jamhuri , timu ya Gairo itakutana na TRA, Ikulu dhidi ya Afya, Maliasili na Mambo ya Nje na Uchukuzi itatoana jasho dhidi ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro.
Kundi la pili katika uwanja huo huo, timu ya Mambo ya Ndani itachuana dhidi ya CRDB, Tanesco itacheza na Mahakama na Ulinzi dhidi ya NFRA.