Afya yaelemewa wagonjwa, majeruhi wa ajali
WIZARA ya Afya imesema imeelemewa na wagonjwa na majeruhi wa ajali hasa za barabarani.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema hayo jana alipofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kuwapa pole majeruhi wa ajali iliyotokea juzi Mzakwe katika Manispaa ya Dodoma wakati basi la abiria la Arusha Express lilipogongana na lori la mchanga.
“Sekta ya afya tunaelemewa na mzigo mkubwa wa wagonjwa wa ajali hususani ajari za barabarani.
Kwa mfano ukimhudumia huduma ndogo majeruhi unagharamia shilingi 150,000 na katika majeruhi hawa ni mmoja tu alikuwa na bima ya afya,” alieleza Ummy.
Alisema matibabu makubwa kwa majeruhi wa ajali yanagharimu Sh 600,000 wakati akihitaji kuwekewa vyuma inagharimu Sh milioni mbili.
Ummy alisema katika kuharakisha utoaji wa huduma za afya kwa majeruhi wa ajali za barabarani, Kitengo cha Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza kitaimarishwa ili kijumuishe na masuala ya ajali.
“Tunakwenda kuimarisha Idara ya Magojwa Yasiyo ya Kuambukiza ili kuingia ajali na afya ya akili, tunataka ajali iweze kupewa kipaumbele, tunajua sio wajibu wetu kuzuia ajali, bali tuna wajibu wa kuhakikisha tunatoa msaada wa haraka kwa majeruhi wa ajali,” alisema Ummy.
Amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Afya ahakikishe kitengo cha dharura katika sekta ya afya kinakuwa na mwitikio wa haraka inapotokea ajali ili kuokoa maisha ya watu.
“Naona kunakuwa na uharaka kwenye majanga na dharura kukitokea magonjwa ya Ebola na mengine ya mlipuko, nataka kuwepo na mwamko wa haraka wa kuwahudumia majeruhi inapotokea ajali, tukifanya hivyo tunaweza kuokoa maisha ya watu wengi,” alibainisha.
Alihimiza wataalamu wa afya waendelee kutoa matibabu kwa majeruhi 11 waliotokana na ajali ya juzi hata kama hawatakuwa na fedha za kulipia matibabu.
“Niwashukuru watumishi hospitali ya rufaa ya mkoa kwa kazi nzuri ya kutoa huduma kwa wagonjwa waliopata majeraha kwenye ajali ya basi la Arusha Express,” alisema.
Idadi ya waliofariki dunia kutokana na ajali hiyo imefikia saba baada ya mmoja kupoteza maisha wakati akitibiwa.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Ibenzi Ernest alisema majeruhi aliyekuwa amevunjika miguu na kupata majeraha makubwa kifuani, amefariki wakati akitibiwa.
Dk Ernest alisema majeruhi mmoja alihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa.
“Kwa sasa hapa tumebakiwa na wagonjwa 11 ambao wanaendelea na matibabu, majeruhi tisa tumewaruhusu baada ya kuwa hali zao zimeimarika na kuwa nzuri,” alisema.