AGRA yatangaza mkakati wa kubadili kilimo Afrika

AGRA yatangaza mkakati wa kubadili kilimo Afrika

TAASISI ya Mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRA) imezindua mkakati mpya wa miaka 5 unaolenga kuanzisha njia mpya ya kufanya kilimo katika bara hilo kuwa cha kisasa lakini pia kusaidia serikali kuweka mazingira wezeshi kwa ushiriki wa sekta binafsi katika kuleta mabadiliko kwenye kilimo.

Mkakati huo ambao utekelezaji wake utagharimu dola milioni 550 ulizinduliwa kweye kongamano la 12 la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRF) Kigali Rwanda hivi karibuni.

Taarifa ya mkakati huo uilitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya AGRA, Hailemariam Desalegn  ambaye  alizitaka serikali zote kushirikiana  kuhakikisha uwapo wa mifumo thabiti ya kilimo ili kujihakikishia usalama wa chakula na ubora wake.

Advertisement

Alisema katika utendaji kazi wake, AGRA imebaini haja ya kuwa na mkakati huo  hasa kwa kuwa na uhakika na mifumo ya mbegu itakayochochea uzalishaji wa hali ya juu  kwenye kilimo.

Aidha alisema mkakati huo ambao utawezesha  upatikanaji wa mbegu bora  na pembejeo za uhakika utasaidia serikali nyingi  kuona njia  na fursa za kuleta mabadiliko ya mfumo wa chakula, kusaidia wakulima na kuvutia uwekezaji hasa kutoka kwa vijana ambao ndio nguvu kazi inayoweza kuleta tafsiri mpya ya ajira mashambani.

Mwenyekiti huyo pia alizitaka serikali za kiafrika kuhakikisha zinashirikiana na sekta binafsi kubadili mnyororo  wa kilimo kwa kuhakikisha kwamba  mkulima ana soko la uhakika la ziada yake na pia vijana wanajihusisha na kilimo kwa kuwa na kilimo biashara.

Alisema mkakati huo wa AGRA  wa kuleta mabadiliko ya kilimo, taasisi ya AGRA itatoa msaada kwa sekta kadhaa kwa kujenga masoko ya kilimo jumuishi kwa kuongeza ushindani wa watendaji wa ndani.

Akielezea mkakati huo, Rais wa AGRA, Agnes Kalibata alisema kuwa umeundwa kwa namna ambayo inaakisi maisha ya kila siku ya kila mtu.

Aliongeza kuwa mkakati huo mpya unalenga kubadilisha maisha ya wakulima na kuwasaidia kupata mbegu ambazo zinaweza kubadilisha maisha yao.

Naye , Waziri wa Kilimo wa Burkina Faso Innocent Kiba akizungumzia mkakati huo mpya alisema kuwa maeneo kama vile ufugaji wa kuku yatahitaji kuimarishwa katika mkakati huo mpya kwa vile bado ni sekta inayohitaji kuangaliwa sana nchini mwake.

Mkakati huo mpya unaanza kutumika mwaka ujao wakati ambapo Mkutano wa AGRF pia utabadilishwa jina na kuwa Mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika.