Ahimiza Jumuiya Wazazi kutoa uongozi utakaosimamia maadili

Ahimiza Jumuiya Wazazi kutoa uongozi utakaosimamia maadili

VIONGOZI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametakiwa kuweka viongozi watakaopinga vitendo vya udhalilishaji, ukiukwaji wa maadili na ndoa za jinsia moja.

Wajumbe wa mkutano huo pia wameaswa kufanya uamuzi wa busara wa kuchagua viongozi ambao watatengeneza timu bora ndani ya miaka mitano itakayoimarisha chama na jumuiya hiyo.

Akizungumza jana jijini hapa kwenye Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dodoma, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Gilbert Kalima alisema moja ya dhima na jukumu la jumuiya hiyo ni kuhakikisha inapinga vitendo vya udhalilishaji na ukiukwaji wa maadili, suala linalotakiwa kubebwa na viongozi hao.

Advertisement

“Tunatakiwa kuweka viongozi ambao watahakikisha jumuiya yetu inakuwa kiongozi katika kupiga vita unyanyasaji wa kijinsia, kupiga vita masuala ya ndoa za jinsia moja, kupiga vita ukiukwaji wowote wa maadili katika nchi yetu, kwa kufanya hivyo tutakuwa tunatekeleza wajibu wetu na kanuni ya jumuiya yetu,” alisema.

Aliwataka wajumbe wa mkutano huo wa uchaguzi mkuu kufanya uamuzi wa busara wa kutengeneza timu ambayo katika kipindi cha miaka mitano itajipanga na kufanya kazi ipasavyo ya kuimarisha chama.

Alisema uchaguzi huo ni wa kutengeneza safu ya kukipatia ushindi Chama Cha Mapinduzi katika chaguzi mbalimbali ikiwemo uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Mkipiga kura mkumbuke kwamba mnatengeneza viongozi watakaotuongoza kwenye ushindi wa CCM mwaka 2025 na ushindi wa CCM katika chaguzi zozote zitakazofanyika,” alisema.

Alitaka katika kipindi cha miaka mitano ijayo jumuiya hiyo iweke mikakati ya kujiimarisha kiuchumi. “Mjielekeze katika kuweka mipango na mikakati ya kuhakikisha jumuiya yetu inaondoka hapa ilipo na kujiimarisha kiuchumi kadri inavyowezekana,” alisema.

Kalima alisema kwa miaka mitano ijayo wanajumuiya wahakikishe chama kinakuwa imara zaidi kwa kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.

“Jumuiya iunge mkono jitihada zote zinazofanywa na serikali kuleta maendeleo kwa wananchi, tumuunge mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Dk Damas Mukasa alihimiza wanachama kuendelea na umoja walioonesha wakati wa uongozi wake ili kusimamia sera ya jumuiya na uchumi.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *