Ahimiza wananchi kuendelea na sensa

MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Ahmed Abbas amehimiza wananchi mkoani humo wahesabiwe kwa kuwa kazi hiyo inaendelea.

Abbas alisema jumatano ofisini kwake mjini Mtwata kuwa wameyafikia maeneo yote waliyokusudia kuanza nayo siku ya ufunguzi wa sensa Agosti 23 mwaka huu.

Alisema makarani wa sensa wanaendelea na kazi na akahimiza wananchi mkoani humo waendelee kuhesabiwa na endapo yeyote atakuwa na changamoto ya kumfanya asiwepo nyumbani aache taarifa zake ili makarani wa sensa wakifika wazikute.

Advertisement

Abbas alisema pia ni muhimu wananchi waache na namba ya simu zisaidie kuwasiliana na makarani kama watahitaji ufafanuzi.

“Kubwa nawashukuru wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwa kujitokeza na kuitikia zoezi hili na tuendelee mpaka tutakapolikamilisha ambapo zoezi litaendelea kwa siku saba zaidi,” alisema na kuongeza:

“Wananchi watambue kuwa Agosti 23, mwaka huu ndiyo ilikuwa tarehe elekezi au rasmi ya kuanza kwa zoezi na zoezi hili linaendelea kwa siku saba kwa sababu hatuwezi kuwahesabu watu kwa siku moja nchi mzima,” alisema.