Ahimiza wenye ulemavu kuchangamkia mikopo

OFISA Elimu Maalumu wa Jiji la Dodoma, Issa Kambi amewahamasisha watu wenye ulemavu kujiunga kwenye vikundi ili waweze kupatiwa mikopo ya asilimia mbili inayotolewa na halmashauri badala ya kukaa majumbani kusubiri misaada kutoka kwa wahisani.

Alisema hayo jana wakati akizungumza na wadau wa elimu jumuishi wakiwemo wazazi na walezi wanaoishi na watoto wenye ulemavu kwenye kongamano lililofanyika Dodoma.

Kambi alisema badala ya kukaa majumbani na kusubiri misaada, ni wakati wao sasa kuchangamka na kuunda vikundi ili fursa hiyo ya mikopo inayotolewa waweze kuipata.

“Napenda niwaambie wazazi na walezi mnaoishi na familia na watoto wenye ulemavu kuwa fedha zipo, kila zinapotolewa bado zinabaki, hivyo niwasihi muunde vikundi ili mpate.

Aliongeza: “Msikae tu huko majumbani kusubiri mikopo mletewe bali muunde vikundi na mtoke kuifuata kwenye halmashauri zenu ambazo karibu nchi nzima zinakopesha makundi mbalimbali mkiwemo nyinyi, vijana na wanawake.”

Kambi pia amezionya familia zinazofanyiwa ukatili dhidi ya watoto kutokubali kukaa bila kutoa taarifa, washirikiane na serikali kufichua vitendo hivyo kwa ajili ya kuvikomesha.

Kwa upande wake, Mratibu wa Elimu Jumuishi Jiji la Dodoma na Bahi, Jane Mgidange alisema bado kuna kiwango cha chini sana cha usajili wa watoto wenye ulemavu na kwamba hiyo inatokana na miundombinu ya shule isio rafiki pamoja na idadi ndogo ya walimu wataalamu.

Alisema ofisi ya elimu jumuishi imeona vyema kuisaidia serikali kwa kuanzisha mpango huo wa uhamasishaji wa jamii, kutoa mafunzo kwa walimu, kujenga au kukarabati miundombinu ili kupata mazingira rafiki ya kujifunzia, kujenga vituo vya usaidizi wa kielimu, upimaji na tathmini ya ulemavu pamoja na kufanya ushawishi wa sera na mtaala bora unaokidhi matakwa yote.

Serikali imeombwa kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na taasisi na mashirika mbalimbali katika kutafiti na kuwaibua watoto wenye ulemavu majumbani.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x