DAR ES SALAAM: “Azam hawezi kutufikia tena, mpinzani aliyebaki ni Yanga ambaye na yeye tunataka kumfunga na kumpita kwa alama sita. Ni mechi ambayo tunaitaka kweli kweli, kuanzia kwa mashabiki, benchi la ufundi, wachezaji na viongozi ndio hata hatulali,”
Ndivyo alivyonukuliwa Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally katika Mkutano wake na wanahabari kuelekea mchezo wao wa ‘Kariakoo Derby’ watakapomenyana dhidi ya kikosi cha Yanga kuwania ubingwa Ligi Kuu Tanzania.
–
“Tumewekeza zaidi kwenye kuwafurahisha mashabiki wetu, Jumapili ya Novemba 5, 2023 tunataka kuwafurahisha. Na anayeshinda mchezo huo ndio atatawala nchi hadi tukikutana tena,” amesema Ahmed.
Amesema “Tumecheza mechi ngumu lakini mechi ya Jumapili ni ngumu kuliko zote hii ni kutokana na utani uliopo pamoja na ubora wa timu yao. Tunaona namna wachezaji wao wanajituma. Mechi yetu dhidi yao ni ngumu kweli kweli, mechi ya kipimo cha mpira wa nchi haiwezi kuwa nyepesi.”
Aidha, kiongozi huyo amewaasa mashabiki wa klabu hiyo kijitokeza kwa wingi katika mchezo huo ili kuwapa nguvu wachezaji wao, sambamba na hayo amewaasa kuwa watiifu kwa kuzingatia kampeni ya kuhamasisha vitendo vya kiungwana michezoni ‘Fair play’.
“Mashabiki wetu tuzingatie misingi ya uungwana na ustaarabu, tujitahidi tushangilia na kutaniana kwa heshima ili kuepusha vurugu. Tuendeleze Utanzania kwa utu na upendo.” Amesema Ahmed.
Comments are closed.