Ahueni kwa mpangaji kodi ya zuio ikirudishwa TRA

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba

SERIKALI imefuta utaratibu wa kodi ya zuio itokanayo na pango kukusanywa na mpangaji na badala yake jukumu hilo limerejeshwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa utaratibu utakaobainishwa kwenye kanuni.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ameyasema hayo leo Septemba 20, 2022 bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu.

“Napenda kusisitiza kuwa kodi ya zuio ya pango siyo ya mpangaji bali inapaswa kulipwa na mpangishaji ambaye ndiye anapokea mapato kutokana na uwekezaji au biashara ya kupangisha,” amesema.

Advertisement

Amesema utaratibu huo ulikuwa ukitumika kwa muda mrefu kwa wafanyabiashara au mashirika.

Bunge la bajeti liliifanyia marekebisho Sheria ya Kodi ‘The Income Tax Act R.E 2019 ‘ na kufuta kifungu cha 82(2)(a) kilichokuwa kimetoa maelekezo kuwa wanaopaswa kulipa Kodi ya zuio ‘withholding tax ya 10’ pango ni wale tu wanaopanga nyumba kwa madhumuni ya biashara.

Marekebisho hayo ya sheria yalianza kufanya kazi Julai mwaka huu 2022 pamoja na bajeti ya Serikali kabla ya leo kufutwa rasmi na utaratibu wa awali kurejeshwa.