Ahukumiwa kifo kwa kumuua mkewe

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imemtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, Dibron Saidi kwa kosa la kumuua mkewe, Herieth Justine kwa kumchoma na kisu mara tatu.

Hukumu hiyo imesomwa leo na  Hakimu Mkazi Mkuu, Evodia Kyaruzi aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo na kusema kuwa mahakama imeona hoja zilizotolewa na mshitakiwa wakati akitoa utetezi hazikuwa na ukweli.

Alisema kuwa mshitakiwa alijitetea kuwa alimchoma kisu, Herieth kutokana na hasira alizokuwa nazo kwa kujibiwa maneno ya karaha, baada ya kumfumania akiwa anafanya mapenzi na mwanaume mwingine uchochoroni.

Hata hivyo Hakimu alihoji aliwezaje kuvumilia kumchoma alipokuta akifanya hicho kitendo na amchome kwa maneno aliyokuwa akitoa marehemu?

Hakimu alihoji pia kuwa wakati alipomfumania kulikuwa na purukushani, ambayo alidai ilidumu kwa dakika kumi kabla ya mwanaume aliyemfumania kukimbia, kwa nini hakumchoma muda huo kama alikuwa na hasira.

Pia alisema mshitakiwa alidai kuwa alimchoma kisu marehemu mara moja, lakini ripoti ya uchunguzi wa kitabibu pamoja na maelezo ya shahidi namba tatu ambaye alimshuhudia mshitakiwa akiwa anamchoma kisu pamoja na shahidi namba nne ambaye alikabidhiwa mwili kwa ajili ya mazishi yanaonesha alimchoma kisu mara tatu.

Vilevile alisema kuwa mshitakiwa alidai kuwa marehemu aliteleza katika ganda la ndizi na kuangukia katika kisu ambacho alikuwa amekishika, lakini haikuwa kweli.

Hivyo alisema kwa hoja hizo pamoja na ushahidi uliotolewa na mashahidi sita upande wa mashitaka unajitosheleza kumtia hatiani kwa kosa la kumuua, Herieth kwa kukusudia.

Katika kesi hiyo inadaiwa kuwa Machi 11, 2018 eneo la Vingunguti Majengo, Dibron Saidi alimuua, Herieth Justine kwa kumchoma kisu mara kadhaa kwa madai kuwa alimfumania na yeye mwenyewe  kujaribu kujiua kwa kujichoma na kisu bila mafanikio.

Habari Zifananazo

Back to top button