Aiahidi Yanga ng’ombe watano

MWANACHAMA wa klabu ya Yanga kutoka mjini Geita, Husein Makubi (Mwananyanzala) ameahidi kutoa zawadi ya ng’ombe watano kwa timu ya Yanga baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 5-1 dhidi ya Simba SC.

Ikumbukwe Yanga ilipata ushindi huo katika mchezo namba 64 wa ligi kuu ya NBC uliochezwa Novemba 5, 2023 katika uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Mwananyazala ameahidi zawadi hiyo mbele ya waandishi wa habari mjini Geita na kueleza amechukua uamuzi huo kwani ushindi mkubwa uliopatikana dhidi ya watani zao Simba umeandika historia kubwa.

“Nimefurahishwa na timu yangu ya Yanga, kwa kazi nzuri iliyofanya ya kumfunga mtani magoli matano, kutokana na kazi vijana waliyofanya nzuri, mimi nikiwa shabiki wa Yanga kindakindaki naahidi kuwapa ng’ombe watano.

“Ng’ombe hao watano ni wakubwa makisai, ng’ombe hao nitawasiliana na uongozi wa Yanga, na nitajua nitawafikisha kwa njia gani.

” Amesema Mwananyazala.

Aidha amempongeza Rais wa klabu ya Yanga, Mhandisi Hersi Said kwa uongozi wake makini na uliotukuka kwani ndani ya muda mfupi wa uongozi wake timu imepata mafanikio makubwa kwenye mashindano ya ndani na nje ya nchi.

“Kwa hiyo mimi nampongeza sana, pia kocha tuliyenaye anafanya kazi nzuri, vijana sasa hivi wanacheza mpira mzuri sana utafikiri wamezaliwa tumbo moja, mpaka wamefikia hatua ya kutufurahisha nchi nzima.”

Mwananyanzala ameahidi kuendelea kuunga mkono zawadi ya Rais Samia Suluhu kwa kununua kila goli linalofungwa na wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya klabu bigwa barani Afrika.

Amewaomba wachezaji kutobweteka na ushindi walioupata dhidi ya Simba Sc badala yake waendelee kucheza kwa kujituma na kwa kiwango cha juu ili mwenendo wa klabu uendelee kuwa bora zaidi.

Habari Zifananazo

Back to top button