Aipongeza serikali utekelezaji hoja za CAG

SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema katika miezi saba serikali imetekeleza asilimia 48 ya maagizo ya Bunge yaliyotolewa kuhusu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2020/21.

Akizungumza bungeni Dodoma jana mara baada ya kamati tatu za Bunge kuwasilisha taarifa ya utekeleza wa serikali kuhusu maagizo ya Bunge yanayohusu hoja za CAG, Dk Tulia alisema serikali inastahili pongezi kutokana na hatua hiyo ya utekelezaji. Alisema Bunge hilo lilitoa maagizo hayo kwa serikali Novemba, mwaka jana.

Alieleza kuwa tangu maagizo hayo yatolewe takribani asilimia 48 ya maagizo ya Bunge kwa serikali yamefanyiwa kazi hivyo wabunge watambue kuwa serikali inayafanyia kazi maagizo yanayotolewa na mhimili huo wa dola. Dk Tulia alisema kwa hali ilivyo hadi Novemba mwaka huu huenda serikali ikatekeleza maagizo hayo ya Bunge kwa asilimia nyingi zaidi.

Alisema Bunge limeamua taarifa za maagizo ya Bunge kuhusu hoja za CAG kuanzia sasa zisomwe wazi bungeni na si kama zamani ambapo zilikuwa zinasomwa kwenye vikao vya kamati za Bunge. “Hii itaondoa yale maneno kwamba taarifa za CAG zinawasilishwa bungeni lakini Bunge halizifanyii kazi. Tumekuwa tukitoa maelekezo serikali na kwa taarifa hizi inaonesha serikali inayachukulia kwa uzito na kuyafanyia kazi,” alisema Dk Tulia.

Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC), Halima Mdee alisema serikali imetekeleza kwa asilimia 42 maagizo ya Bunge yaliyotolewa kuhusu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mdee alisema kwa mujibu wa mchanganuo kati ya maagizo hayo asilimia 32 yako kwenye hatua ya utekelezaji, asilimia tisa hayajaanza kutekelezwa na asilimia tatu yamepitwa na wakati. Alisema bado kuna changamoto ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na CAG katika halmashauri.

Alitaja maeneo ambayo bado yanahitaji kufanyiwa kazi kuwa ni mfuko wa mikopo kwa vikundi vya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu, upatikanaji wa ruzuku ya maendeleo katika mamlaka za serikali za mitaa na uwekevu na tija katika uwekezaji wa mitaji ya umma.

Habari Zifananazo

Back to top button