Airport yatwaa ng’ombe mashindano ya Polisi Jamii

TIMU ya soka ya Airport kutoka Kata ya Katubuka Manispaa ya Kigoma Ujiji, imefanikiwa kuwa bingwa wa mashindano ya Polisi Jamii yanayoandaliwa na ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, lengo likiwa kutoa elimu na kuhamasisha jamii kushiriki kwenye ulinzi na usalama wa maisha yao na mali zao.

Timu ya Airport imefanikiwa kutwaa ubingwa huo katika mchezo wa fainali wa mashindano hayo, baada ya kuibugiza timu ya Mwandiga kwa mikwaju ya penalti 5-4 na hivyo kunyakua zawadi ya Ng’ombe mmoja na fedha taslimu Sh 200,000.

Timu ya Mwandiga iliyoshika nafasi ya pili ya mashindano hayo imepata zawadi ya seti moja ya jezi na pesa taslimu Sh 150,000.

Kamanda wa polisi mkoa Kigoma Filemon Makungu akizungumza kwenye mchezo wa fainali wa mashindano ya soka ya Polisi jamii Manispaa Kigoma Ujiji. (Picha zote na Fadhil Abdallah.)

Nafasi ya tatu ya mshindi wa mashindano hayo ambayo yalikuwa yanafanyika kwenye Uwanja wa Kawawa Ujiji Mjini Kigoma imeenda kwa timu ya Kitongoni, ambayo ilipata zawadi ya fedha taslim shilingi 100,000.

Akizungumza wakati wa fainali za mshindano hayo, Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Philemon Makungu alisema kuwa mwisho wa mashindano haya ndiyo mwanzo wa maandalizi ya mashindano ya mwakani na kuahidi kuboresha na kuongeza zawadi zaidi.

Kamanda Makungu alisema kuwa mashindano hayo yamepata mafanikio kwa kuwafikia watu wengi na kutoa elimu na hamasa iliyokusudiw,a lakini imeweza pia kuendeleza michezo kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Kigoma.

Athuman Saidi Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji mashindano ya Polisi Jamii Manispaa ya Kigoma Ujiji akitoa maelezo kuhusu mashindano hayo, wakati wa mchezo wa fainali.

Akitoa maelezo kuhusu mashindano Mwenyekiti wa mashindano, Athuman Saidi ambaye ni Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kigoma, alisema kuwa jumla ya timu 16 zilishiriki mashindano hayo ambayo yaliendeshwa kwa makundi hadi kufikia mchezo wa fainali.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button