Ajali ya basi, lori yaua Morogoro

MTU mmoja amefariki dunia na wengine saba  kujeruhiwa, baada ya basi la abiria lililokuwa likitokea Musoma kuelekea Dar es Salaam kugongwa na lori la mafuta.

Ajali hiyo ilitokea majira ya saa tano usiku wa Juni 18,mwaka huu, eneo la  Kingolwira, Manispaa ya Morogoro barabara kuu ya Morogoro – Dar es Salaam.

Basi hilo lenye namba za usajili T 728 EBT  mali  Kampuni ya Johanvia Express, liligongwa na lori  la kubeba mafuta lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea mikoani.

Advertisement

Kabla ya kutokea ajali hiyo, katika eneo hilo ilitokea ajali nyingine iliyohusisha  lori aina ya Fuso lenye  namba za usajili T 883 DMA, likiwa limebeba matenga ya nyanya kupelekwa Dar es Salaam, likitokea mkoani Iringa,  baada ya kupoteza uelekeo na kupinduka.

Wakati inatokea ajali ya basi na Lori la mafuta,  askari wa Kikosi cha usalama barabarani walikuwa wakiwahudumia majeruhi wa Fuso na  dakika chache ikakotokea ajali hiyo ya  basi na Lori, hivyo  kuzua taharuki eneo hilo.

Akizungumza Zuri Barnabas aliyesafiri na basi hilo, alisema ajali ilitokea baada ya dereva wa lori la mafuta kuhama upande wake na kulifuata basi na kuligonga sehemu ya  mbele na ubavuni, hivyo  basi lao kwenda kulalia gari la Polisi iliyoegeshwa pembezoni, wakati walipokuwa wakiihudumia abiria wa Fuso.

Aliyefariki papo hapo katika ajali ya basi  hilo ni mtuhumiwa ambaye alikuwa chini ya ulinzi wa askari akipelekwa Dar es Salaam kusikiliza shauri lake.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoji Mkoa wa Morogoro, Emmanuel Ocheing, alisema alijulishwa kutokea kwa ajali hiyo na Kamanda wa Polisi mkoa huo, Alex Mkama majira ya saa sita usiku,  ambayo ilihusisha basi la abiria na lori la mafuta.

Alisema walifika eneo la tukio na kuhakikisha usalama na tahadhari zote zinachukuliwa kwa kuwa ajali hiyo ilihusisha lori la mafuta na walifanikiwa kuliondoa tanki hilo na kubakia kichwa cha lori, ili ikiepusha madhara.