Ajali ya Fuso yaua ‘wakandarasi’ 5

KIGOMA; WATUMISHI watano wa kampuni ya Tropical State Grid Co.Ltd, inayotekeleza Mradi wa Umeme Vijijini (REA), wilayani Uvinza mkoani Kigoma, wamefariki dunia na wengine nane wamejeruhiwa baada ya gari waliyokuwa wakitumia kuacha njia na kupinduka.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Filemon Makungu amesema ajali hiyo ilitokea Juni 9, 2024  na kwamba ajali ilitokea baada ya gari aina ya Fuso wanayotumia wakandarasi hao wanaotekeleza mradi wa REA, lenye namba za usajili T 224 BZD kuacha njia na kupinduka, ilipokuwa ikitoka Kijiji cha Lubisi kuelekea Kijiji cha Rukoma.

Amewataja waliokufa ni Samwel Kashoka (30), Dismas Ntayomba (21), Enock Chimanguli (42),  Benson Thomas (25) na   Juma Bashiru (29), ambao ni mafundi.

Amewataja waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo kuwa ni Said Ramadhani (45), Venance Mabula (24) na Elizabeth Mero (30) Msimamizi wa mradi, ambao walitibiwa na kuruhusiwa baada ya hali zao kuwa nzuri.

Kamanda Makungu amesema kuwa watu watano wamelazwa baada ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kigoma Maweni, kutoka Kituo cha Afya Rukoma, Wilaya ya Uvinza kutokana na hali zao kuhitaji matibabu zaidi.

Amewataja majeruhi ambao bado wamelazwa wakiendelea na matibabu Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kigoma Maweni kuwa ni  Hussein Fadhili (24),  Yassin Athumani (19),   Mtala Joseph (24)  Victor Joseph (31), na Claudiao Mwalima (31)

Habari Zifananazo

Back to top button