Ajali ya gari yaua watatu Mtwara

MTWARA: WATU watatu wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha gari ndogo Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.

Akitoa taarifa hiyo leo kwa  waandishi wa habari, Kaimu Kamishna wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara  Mtaki Kurwijila amesema ajali hiyo imetokea Oktoba 29, 2023 majira ya saa 11:50 usiku katika eneo la Mikindani mlima wa soda Barabara ya Mtwara Lindi wilayani humo.

‘’Ajali hiyo imesababisha vifo vya abiria watatu wa gari hilo na majeruhi watatu waliyokuwa katika gari na mpanda pikipiki mmoja’’amesema Kurwijila

Aidha gari hiyo ilikuwa imebeba abiria saba aina ya Toyota Alphad lenye namba za usajili T404 EDB mali ya Abdallah Ahmad iliyokuwa ikiendeshwa na dereva Yahya Juma (35) mkazi wa manispaa ya mtwara Mikindani mkoani humo.

Amesema gari hilo liligonga kwa nyuma gari ya kampuni ya kuzalisha saruji (Dangote) mkoani humo lililokuwa limeengeshwa pembeni kwa barabara baada ya kupata hitilafu na kisha kugonga pikipiki aina ya TVS ambayo haijafahamika namba zake za usajili iliyokuwa ikiendeshwa na Diocles Peter (25) mkazi wa manispaa hiyo.

Kaimu Kamanda huyo amewataja  marehemu hao kuwa ni Mwanaidi Selemani (51), Nialy Ally (32) wakazi wa manispaa hiyo pamoja na Mohamed Mfaume (60) mkazi wa Ziwani Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.

‘’Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa  dereva wa gari ndogo na kushindwa kuchukua tahadhari ya kutosha barabarani, dereva wa gari hilo dogo alitoweka kusikojulikana huku juhudi zikiendelea kufanyika ili kuhakikisha dereva huyo anakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria’’,amesema Kurwijila

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button