Ajali yaua watano, yajeruhi kumi

WATU watano wamepoteza maisha na wengine 10 wamejeruhiwa baada ya basi dogo aina ya Toyota Coaster kugongana uso kwa uso na lori la mizigo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama alisema ajali hiyo ilitokea jana saa moja asubuhi wakati basi hilo likitoka Mbeya kwenda Dar es Salaam.

Kamanda Mkama alisema ajali hiyo ilitokea katika Barabara Kuu ya Morogoro- Iringa eneo la Iyovi, mpakani mwa Kijiji cha Igagala Luhembe katika Tarafa ya Mikumi wilayani Kilosa katika Mkoa wa Morogoro.

Advertisement

Alisema ajali hiyo ilihusisha basi dogo lenye namba za usajili T 938 DVQ lililogongana na lori la kubeba mafuta lenye namba za usajili T 693 DMF lenye tela namba za usajili T 586 DKR lililotoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Kamanda Mkama alisema watu watano waliopoteza maisha ni wanaume watatu na wanawake ni wawili na majina yao hayajafahamika na pia jina la dereva wa basi dogo halikuweza kufahamika.

Alisema dereva wa basi dogo huyo alikimbia baada ya kusababisha ajali hiyo na wanaendelea kumtafuta achukuliwe hatua za kisheria.

Kamanda Mkama alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi dogo kuamua kulipita lori lililokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari na kusababisha kugongana uso kwa uso na lori.

Aliwataja majeruhi wa ajali hiyo ni Abi Peter Mwansepe (52) mkazi wa Mbeya, Said Haji Mohammed (48) mkazi wa Zanzibar, Michael Kabota (30) mkazi wa Sumbawanga na John William Kameta (42) mkazi wa Tabata Kimanga, Dar es Salaam.

Majeruhi wengine ni Hafidh Abdallah (26) mkazi wa Maili Moja Kibaha, Denis John Msisiri (46) mkazi wa Mbeya, Alex Makongolo Magoma (45) mkazi wa Kihonda Morogoro, Victor Amanyiyisye Mwaipopo (69), mkazi wa Mbeya, Jumanne Kondo Seleman (35) mwingine ambaye hakujulikana jina lake.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya St Kizito Mikumi, Dk Steven Mbilinyi alisema walipokea miili ya watu watano waliopoteza maisha katika ajali hiyo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *