PWANI: WATU watatu wamefariki na wengine wawili kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugonga gari lililokuwa limeegeshwa barabarani, katika eneo la Mbwewe, Chalinze, wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.
Akitoa taarifa hiyo Kwa vyombo vya habari, mjini Kibaha, Kamanda wa polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo, alisema ajali hiyo imetokea Desemba 28, 2023 majira ya saa 11: 45 alfajiri.
Amesema gari lenye namba za usajili T. 395 DWE aina ya Alphard likiendeshwa na dereva, Mohamed Athuman (40) aligonga kwa nyuma gari lenye namba za usajili T.300. CLE/ T.399 AUP aina ya Faw lililoegeshwa pembezoni mwa barabara na kusababisha vifo vya watu hao papo hapo.
“Watu watatu akiwemo mtoto mchanga wamefariki baada ya gari lao kugonga gari jingine lililokuwa likiendeshwa na dereva, Alphonce Bosco (55) kwa nyuma na kusababisha vifo na majeruhi wawili”alisema
Kamanda amewataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Zakia Mohamed (36), Nadim Nurdin (miezi 8) na Goleth (23) wote wakiwa wakazi wa Kabuku Tanga na majeruhi, Mohamed Athuman (40) na Alice Sangule (08).
Aidha amesema uchunguzi umebaini chanzo cha ajali ni dereva wa gari T.300. CLE/ T.399 AUP aina ya Faw kuegesha gari kando ya barabara pasipo kuweka alama yeyote ya tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara.
“Chanzo Cha ajali ni uzembe tu..jeshi la polisi linatoa rai kwa madereva kuendelea kuchukua tahadhari na kuheshimu sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazosababishwa na uzembe hususani katika kipindi hicho cha sikukuu za mwisho wa mwaka”alisema