Ajali za barabarani zapungua kwa asilimia 35 Geita

GEITA: JESHI la Polisi mkoani Geita limeeleza matukio ya ajali za barabarani mkoani humo yamepungua kwa asilimia 35 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kutoka ajali 74 mwaka 2022 hadi ajali 48 mwaka 2023.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Safia Jongo amebainisha hayo wakati akizungumzia mafanikio ya jeshi hilo kwa kipindi cha Januari hadi Novemba mwaka 2023.

Kamanda Jongo amesema mafanikio yanatokana na juhudi za jeshi la polisi kuzuia ajali za barabarani kwa kuchukua hatua sambamba na kutoa elimu kwa madereva wanaokiuka sheria za barabarani.

Amesema takwimu zinaonyesha mpaka Desemba 2023 kuna upungufu wa ajali 26 zilizosababisha vifo na majeruhi kwa ulinganifu wa ajali zilizoripotiwa mwaka 2022 na zile zilizoripotiwa mwaka 2023.

“Kuelekea mwisho wa mwaka jeshi la polisi Mkoa wa Geita tumeweka mikakati ya kufanya oparesheni mbalimbali, misako na doria ili kuhakikisha kwamba hali ya usalama inatengemaa.”Amesisitiza Kamanda.

Kamanda Jongo ameongeza kuwa jeshi la polisi linaendelea kutekeleza mkakati wa kubaini na kuzuia uhalifu ndani ya Mkoa wa Geita na kuhakikisha jamii inapata elimu ya kutosha ya ulinzi shirikishi.

Amesema mpaka sasa vikundi 360 vya ulinzi shirikishi vimeanzishwa, klabu rafiki kwa jeshi la polisi 328 za kupinga dawa za kulevya na kuzuia ukatili kwa watoto zimeanzishwa mashuleni.

“Jeshi la polisi Mkoa wa Geita tumetoa elimu na tunaendelea kutoa elimu ya dhana ya polisi jamii, elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto na elimu ya usalama barabarani.”

Kamanda ameeleza kwamba, kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2023 jumla ya vipindi vya redio 122 vimetumika kutoa elimu na kata 123 zimepatiwa elimu ya ulinzi shirikishi.

Habari Zifananazo

Back to top button