‘Ajali bodaboda wanaumia mifupa, ubongo’
MKURUGENZI wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) Prof Abel Makubi amesema asilimia 60 ya majeruhi wa ajali hasa bodaboda wanaumia sehemu za ubongo.
Prof Makubi ameyasema hayo katika Mkutano wa Kimataifa wa wataalamu wa ubongo,mishipa ya fahamu na uti wa mgongo ulioandaliwa na MOI kwa kushirikiana na chuo na Hospitali ya Well Cornel iliyopo nchini Marekani leo jijini Dar es Salaam.
“Kwa wastani kwenye idara ya magonjwa ya dharura tunapokea wagonjwa 15 hadi 20 ambao wanatokana na dharura mbalimbali na asilimia 60 zinatokana na ajali na wengi ni bodaboda, tatizo ni kubwa wengi wanakuwa wameumia mifupa na ubongo,”ameeleza.
Amesema mkutano huo wa siku nne unatoa mafunzo ya tiba inayotokana na ajali zinazoumiza ubongo, yatawasaidia wataalamu kuwatibu wananchi walioumia kwa ajali zilizoathiri ubongo na mgongo.
“Wataalamu wanajengewa uwezo kuwatibu kwa umahiri na kupunguza matatizo yanayotokana na ajali tumekuwa tukishirikiana kwa muda wa miaka 12,” amesema.
Amesema kupitia ushirikiano huo, wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi wamekuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana, kufanya tafiti katika maeneno ya tiba ya ubongo na wamekuwa na vifaa vya zaidi ya bilioni moja ambavyo vimewasaidia katika upasuaji wa ubongo.
“Pia tunapata wataalamu kutoka Marekani ni ushirikiano wa faida kwa pande zote mbili kila mwaka tunakutana,” amesema.
Prof Makubi alisema idadi ya wataalamu hao bado ni ndogo, ambapo MOI kuna madaktari bingwa 12 na nchi nzima wako 23 ikilinganishwa na idadi ya Watanzania.
Naye daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, Dk Hamisi Shabani amesema kabla upasuaji wa uti wa mgongo wagonjwa walikuwa wanapelekwa nje lakini sasa wote wanatibiwa ndani.
“Sasa imepatikana hamasa ya madaktari kujifunza, mimi nilikuwa daktari wa tatu walipokuja sasa wako 23, ila sio somo gumu ambalo watu wanatakiwa kukimbia imekuwa rahisi kwetu kuongeza ujuzi tofauti na awali,” amesema.
Amesema wana wanafunzi sita kutoka nje ya nchi na wanne wa ndani ya nchi na kwamba watatumia teknolojia mpya baada ya vifaa kuletwa vya endoscopy, ambapo mgonjwa atakaa saa chache hospitali.
Amesema bado kuna uhaba wa madaktari bingwa, ambapo kwa viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa nchi zinazoendelea daktari mmoja anatakiwa kuhudumia wagonjwa 100,000 kwa mwaka, huku kwa sasa nchini daktari mmoja akihudumia wagonjwa milioni 1.2 kulingana na idadi ya Watanzania .
Prof Roger Hartl kutoka Chuo cha Well Cornel amesema amejifunza mbambo mengi baada ya kuja Tanzania ambayo yamemsaidia kuhudumiwa wagonjwa wake huko Marekani.
“Tumetengeneza mfumo wa kufundisha wataalamu kwa kubadilishana ujuzi wanakuja kwetu na sisi tunakuja kwao ili kuhakikisha tunahudumia wagonjwa kwa namna ya kufanikiwa ,”amesisitiza.