Ajeruhiwa na fisi akienda kuchota maji

JOYCE Sengerema,10, mkazi wa kitongoji cha Mabuki kijiji cha Kiloleli Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga amejeruhiwa na fisi maeneo ya shingoni, kichwani na kwenye mbavu wakati akienda kuchota maji kwenye mto Manonga.

Shangazi wa mtoto huyo Kamwa Maganga akiongea na gazeti hili jana kwenye wodi ya watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambapo amelazwa nakupatiwa matibabu alisema fisi huyo alimjeruhi tarehe 27/05/2023 majira ya saa 12 Alfajiri .

Maganga alisema mara kwa mara huwa wanafuata maji mtoni majira ya asubuhi lakini alishangaa kusikia kelele za watoto kukimbizwa na Fisi huku wakidai Joyce tayari kashambuliwa.

Baba mzazi wa mtoto huyo, Kisiwa Maganga alisema hakuwepo nyumbani alipigiwa simu nakuelezwa tukio la mtoto kujeruhiwa na Fisi huku alimshukuru baba mmoja aliyeitwa Kashindye kumuokoa mwanae.

“Mtoto wangu alibuluzwa na fisi kuelekea vichakani huku akiwa amemng’ata maeneo ya shingoni,ubavuni na kichwani tulimpeleka Hospitali ya Kolandoto wakatupa Rufaa ya kuja Hospitali hii ya mkoa Sasa anaendelea kupata matibabu”alisema Maganga.

Diwani wa kata ya Kiloleli Edward Manyama alisema taarifa ilimfikia mtoto huyo kushambuliwa fisi wakati akifuata maji Mto Manonga akiwa na wenzake wawili na fisi huyo baada ya kung’ata alianza kutembea naye vichakani watu waliona nakuanza kumfukuza Kisha kumuacha kichakani.

Diwani Manyama alisema mtoto huyo ameanza kupata huduma hali yake bado haijawa nzuri aliwaomba maafisa wanyapori Kishapu kuendelea kuwasaka fisi Kama ilivyokuwa miaka ya nyuma walivyoshambulia zaidi watoto na mifugo.

Muuguzi wa zamu kutoka Hospitali ya Rufaa Jesse Samweli alikiri kumpokea mtoto huyo na wameanza kumpatia matibabu .

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi alipotafutwa kuliongelea tukio hilo hakuweza kupatikana Ila ndugu waliliripoti kituo cha polisi wilayani Kishapu.

Habari Zifananazo

Back to top button