Ajira kwa vijana kizungumkuti

SERIKALI imesema licha ya hatua kubwa ilizochukua za kujenga uchumi,  tatizo la ajira kwa vijana  bado ni kubwa.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba akiwasilisha kadirio ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2023/2024 Bungeni Dodoma leo Juni 15, 2023 amesema viwango vya ukosefu wa ajira bado ni vya juu na vinahitaji juhudi zaidi kuvipunguza.

Amesema, utafiti wa Nguvukazi wa mwaka 2020/21 ulibaini kuwa ukosefu wa ajira katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 35 nchini Tanzania imekuwa ikiongezeka kutoka asilimia 12.1 kwa mwaka 2014 hadi aslimia 12.6 kwa mwaka 2020/21. 7

“Tatizo hili la ajira ni kubwa zaidi hasa kwa vijana wa kike ambao ni asilimia 16.7 ikiwa ni mara mbili ya kiwango kwa vijana wa kiume  ambao ni asilimia 8.3”Amesema Mwigulu.

Hata hivyo, amesema serikali imechukua hatua mbali mbali kupunguza tatizo hilo la ajira na kwamba katika Utafiti wa Nguvukazi wa mwaka 2020/21 ulibaini kuwa ukosefu wa ajira kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 15 au zaidi ulipungua hadi asilimia 9.3 kutoka asilimia 10.5 mwaka 2014.

“Kupungua kwa kiwango hiki ni matokeo ya juhudi mbalimbali zilizotekelezwa na Serikali, ingawa viwango vya ukosefu wa ajira bado ni vya juu na vinahitaji juhudi zaidi kuvipunguza,” amesema Mwigulu

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button